Hao Tanzanite yaani mapema tu

Sunday August 11 2019

 

By THOMAS NG’ITU

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite asubuhi ya leo kitakuwa na kazi moja tu, kupata ushindi dhidi ya Zambia ili kubeba taji la CosafaU20, lakini pia kulipa kisasi cha mabao 2-1.

Kocha wa timu hiyo, Bakar Shime ‘Mchawi Mweusi’ alisema wanataka kulipa kisasi na kuondoka na taji la michuano hiyo ya soka la wanawake Kusini mwa Afrika U20.

Zambia iliifunga Tanzania kwenye mechi ya makundi na timu zote kutinga nusu fainali na kila moja kupata ushindi dhidi ya Afrika Kusini na Zimbabwe zilizocheza jana Jumamosi kusaka ushindi wa tatu.

Zambia ilipenya fainali kwa kuifunga Zimbabwe bao 1-0, huku Tanzania ikiwaondosha wenyeji Afrika Kusini kwa mabao 2-0 na asubuhi ya leo zitamaliza ubishi kwenye Uwanja wa Wolfson, mjini Port Elizabeth.

Kocha wa Tanzanite, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ alisema mchezo wa leo dhidi ya Zambia utakuwa mgumu kutokana na matokeo ya awali.

Shime alisema katika mchezo huo wanataka kulipa kisasi baada ya kufanyia marekebisho ya mchezo wa kwanza dhidi ya Zambia.

Advertisement

“Mechi yetu itakuwa nzuri na huu ni mchezo wa marudiano, nimeshawaandaa wachezaji wangu na wapo katika hali nzuri ili tuweze kupata matokeo mazuri,” alisema.

Akizungumzia upande wa majeruhi katika kikosi chake alisema hakuna, lakini isipokuwa atamkosa Irene Kisesa ambaye alipewa kadi nyekundu itakayomfanya akose mchezo huo.

“Hatuna majeruhi na wachezaji wote walifanya mazoezi, pengo lililopo ni mchezji wangu mmoja tu ambaye alipewa kadi nyekundu lakini tayari nimeshajua namna gani ya kufanya,”

Naye nahodha wa Tanzanite, Enekia Kasonga alisema: “Tunahitaji ushindi na tumejipanga vizuri kupitia maelekezo ya makocha wetu, Zambia walitufunga makundi hatutaki iwe hivyo tena.”

Advertisement