UCHAMBUZI: Kenya ikitumia mbinu hizi, Tanzania mbona laini tu

Nairobi.Bado siku moja tu, tushuhudie, Cecafa Derby katika ardhi ya waarabu, pale timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, itakaposhuka kwenye Uwanja wa Jeshi, ulioko Jijini Cairo, kucheza mechi yake ya pili, dhidi ya majirani zao Tanzania ‘Taifa Stars’.

Harambee Stars iliyopoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Algeria ambapo ililazwa 2-0, inategemea kuifunga Taifa Stars kesho, Alhamisi ya Juni 27, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata ya fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), yanayoendelea huko Misri.

Rekodi inaonesha kuwa, mchezo huu hautakuwa mwepesi kwa Kenya, inayoshiriki Afcon, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004, licha ya takwimu kuwabeba dhidi ya Tanzania, inayonolewa na Mnigeria Emmanuel Amunike, inayoshiriki kwa mara ya kwanza tangu 1980.

 Katika michezo 48 iliyowakutanisha mpaka sasa, Kenya imeshinda mara 20 huku Tanzania wao wakishinda mara 14, na sare kati yao ikiwa ni mara 14. Sio hivyo tu, hawajawahi kutana kwenye AFCON tangu mwaka 1969, ambapo matokeo yalikuwa ni sare ya 1-1.

Lakini ifahamike kuwa, mechi ya mwisho kukutanisha timu hizi mbili, ilipigwa mwaka 2017, katika mashindano ya CECAFA, Kenya wakashinda 1-0. Bila shaka kutakuwa na shughuli pevu Jijini Cairo. Je Kenya inahitaji kufanya nini ili washinde?

Ukiangalia rekodi zao za hivi karibuni, utaona kwamba, Harambee Stars wamepoteza mchezo kwa kufungwa bao 2-0, katika mechi tisa. Itabidi mabeki wa Kenya, wafanye kazi kubwa kuwazuia mastraika wa Tanzania hasa, Mbwana Samatta.

Rekodi, inaonesha kuwa Tanzania, imepoteza michezo minne katika nane walizocheza katika siku za hivi karibuni. Sebastien Migne, atahitaji kushambulia kwa nguvu zote, maana hata beki ya Taifa Stars, haiku makini sana.

Katika kushambulia, Harambee Stars, inatakiwa kujenga mashambulizi kuanzia eneo la juu la timu, kwa sababu kama nilivyosema hapo mwanzo, Kombinisheni ya safu ya ulinzi ya Tanzania inayoongozwa na Hassan Ramadhani na Kelvin Yondani, imeonesha kupwaya.

Ushahidi wa mapungufu haya ya safu ya Ulinzi ya Tanzania, ilionekana dhidi ya Senegal ambapo waliruhusu kupigiwa mashuti 24, 10 kati yao yakilenga lango na kama sio uimara wa mlinda lango Aishi Manula, mambo yangekuwa mabaya zaidi kwao.

Yote tisa, kumi ni kwamba, matokeo chanya kwa Harambee Stars, yatategemea umahiri wa wachezaji wake, kuanzia kwenye kujilinda, kutengeneza nafasi na kushambulia, maana kwenye mchezo uliopita waliishia kupiga mashuti manne tu, yote yakienda fyongo.