Fainali ya Chapa Dimba 2019 ni Manyatta United Vs Al-Ahly Leo

Sunday June 23 2019

Mwanasport, Mwanaspoti, Fainali ya Chapa Dimba 2019, Manyatta United Vs Al Ahly Leo

 

By Fadhili Athumani

Meru, Kenya.  Wakati Wakenya wakisubiri kushuhudia mtanange wa kukata na shoka wa Kundi C, kati ya timu ya taifa, Harambee Stars dhidi Algeria kwenye makala ya Afcon yanayoendelea mjini Cairo, huko Meru kutakuwa na fainali nyinyine babkubwa.

Fainali hiyo, inayohitimisha makala ya pili ya mashindano ya kunoa vipajji vya soka nchini, inayodhaminiwa na kampuni ya simu ya Safaricom kwa ushirikiano na ligi kuu ya Hispania, 'La Liga', itakuwa ni kati ya Manyatta United FC na Al-Ahly FC.

Mechi hii ambayo itaamua mbabe wa soka kwa upande wa timu ya Wavulana itapigwa ugani Kinoru, kuanzia saa kumi alasiri. Manyatta United, kutoka kaunti ya Kisumu, ilitinga fainali kwa kuwalaza mabingwa wa kaunti ya magharibi, Lugari Blue Saints, 2-1 kwenye nusu fainali iliyofahamika kama mashemeji derby.

Kwa upande wao, Al-Ahly FC kutoka Rift Valley, walijikatia tiketi ya ufalme wa mwaka huu wa Chapa Dimba, kwa kuwatandika wajanja wa Jiji la Nairobi, South B United 3-2 kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa matokeo ya sare ya 2-2.

Wakati huo huo, kutakuwa na fainali kali ya kusaka bingwa wa makala haya, kwa upande wa akina Dada, ambapo Kitale Queens ya Kitale, itashuka dimbani kuivaa Acakoro Ladies ya Nairobi. Mechi hii itapigwa kuanzia saa nane mchana kabla ya fainali ya wanaume.

Kitale Queens na Acakoro Ladies walitinga fainali baada ya kuwafunga wapinzani wao Barcelona Ladies kutoka Central 6:1 na Changamwe Ladies ya Pwani 4:2 mtawalia katika hatua ya nusu fainali.

Advertisement

Licha ya kubanduliwa katika hatua ya nusu fainali, Lugari Blue Saints, South B United, Barcelona Ladies na Changamwe Ladies, hawakuondoka mikono mitupu, kwani walizawadiwa kitita cha Shilingi 250,000 kila mmoja.

Bingwa wa mwaka huu, kwa kina Dada na wanaume atazawadiwa Shilingi 500,000. Balozi wa mashindano haya ni nyota wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya Hispania, Luis Garcia, ambaye amekuwa akitoa mafunzo kwa vijana hao. Garcia atakuwa dimbani kushuhudia fainali za leo.

 

Advertisement