Ushindani wa namba Harambee Stars wamkuna Cliffton Miheso

Muktasari:

Mara ya mwisho kwa Miheso kuichezea Stars, ilikuwa ni katika mashindano ya Hero Intercontinental Cup, yaliyofanyika huko India.

Nairobi. Kiungo wa Harambee Stars, Cliffton Miheso amesema upinzani uliopo katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ kambini Ufaransa ni mkubwa sana tofauti na miaka ya nyuma.

Stars, imeweka kambi ya siku 19 katika uwanja wa Marcoussis, iliyoko makao makuu ya shirikisho la Rugby la Ufaransa, kwa ajili ya kujiandaa na fainali za mataifa ya Afrika, yatakayofanyika nchini Misri, kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Miheso ni mmoja wa viungo wakabaji sita, waliojumuishwa katika kikosi cha wachezaji 27 cha Stars, kinachonolewa na Mfaransa Sebastien Migne, ambayo baadae itapunguzwa hadi 23 watakaoelekea Misri kushiriki AFCON 2019.

“Sidhani kama nina presha yoyote ile. Tunafanya mazoezi kitimu na kwa ushirikiano mkubwa. Pamoja na ukweli kwamba kila mmoja anapigania nafasi yake kikosini Kocha amekuwa akisisitiza tucheze kitimu zaidi. Hii imefanya ushindani uwe mkubwa zaidi tofauti na timu za huko nyuma," alisema Miheso.

Kiungo huyo wa klabu ya Olimpico Montijo ya Ureno, pia anaamini kuwa michuano hii, itakuwa ni fursa ya wachezaji kuonesha uwezo wao na kujiuza Ulaya, hivyo ni lazima kila mtu apambane kupata namba.

“Niliposhiriki michuano ya kombe la CECAFA mwaka 2013, nilifanikiwa kuvivutia vilabu vingi ndani na nje ya mipaka ya Afrika. Ilikuwa ni fursa ya pekee kwangu, hivi sasa nacheza nchini Ureno, naamini wenzangu pia wanataka kuonesha kipaji chao," alisema.

Mara ya mwisho kwa Miheso kuichezea Stars, ilikuwa ni katika mashindano ya Hero Intercontinental Cup, yaliyofanyika huko India, ambako aliifungia Kenya goli moja.

Harambee Stars ambayo inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza baada ya kuzikosa kwa zaidi ya miaka 15, itacheza mechi mbili za kirafiki ya kwanza, ikiwa ni dhidi ya Madagascar (Juni 7) na ya pili ikiwa ni dhidi ya DR Congo, itakayopigwa Juni 15, Jijini Madrid.

Stars ipo Kundi C, pamoja na majirani zao Taifa Stars (Tanzania),  Algeria na Senegal, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal,  Julai mosi. Mechi zote zitapigwa Cairo, kwenye Uwanja wa June 30.