Yanga wamuita Molinga chemba

MABAO mawili aliyofunga straika wa Yanga, David Ndama Molinga ‘Falcao’ katika mechi dhidi ya Namungo yaliwapa furaha mashabiki huku Kocha Luc Eymael akisema kwamba atampa mkataba mpya.

Baada ya kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo, Molinga aliiambia Mwanaspoti kuwa mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kuheshimu wachezaji wao kwani si rahisi kutoka nchini Ufaransa alipokuwa anaishi kuja kucheza soka la kujifurahisha hapa Tanzania.

Molinga alisema maneno mabaya ambayo mashabiki wa timu hiyo waliyatoa mara baada ya mechi dhidi ya Azam, yalimuuma sana hadi alishindwa hata kulala vizuri kwani muda wote yalikuwa yakimrudia katika kichwa chake.

“Msimu ukimalizika naondoka, wanaweza kusajiliwa wachezaji wengine wazuri zaidi, mashabiki wanatakiwa kuacha tabia ya kuwatolea maneno makali kama walivyofanya kwangu,” alisema.

“Mabao ambayo nimefunga katika mechi dhidi ya Namungo ni majibu tosha kwa mashabiki wote waliokuwa wananibeza na nimewanyamazisha wote kwani nilijikuta nashangaa kuona wananiomba msamaha. Ila ambalo nataka kuwaeleza sina shida nao wala kinyongo chochote ila maneno yao yaliniuma na watambue walinikosea sana,” alisema.

“Unakumbuka nilikuambia kama nitapata muda wa kutosha kucheza katika mechi mfululizo naweza kufunga mabao 15, mpaka msimu ukimalizika au zaidi ya hayo, nadhani unalikumbuka hilo kwani hata katika gazeti lenu mliandika.

“Wengine wamecheza mechi nyingi na muda mwingi kuliko mimi lakini hawajanifikia, sasa fikiria kama ningepata muda wa kutosha kucheza hata mechi tano mfululizo ningekuwa na mabao mangapi muda huu,” alisema.

“Kama ukiangalia vizuri baada ya kufunga nilikuwa na furaha ya aina yake nikashindwa hata kushangilia na wenzangu kutokana na jambo hilo lilitokana na uchungu ambao niliupata kutoka kwa mashabiki kwenye mechi iliyopita, lakini nilikuwa naonyesha ishara ya mgongoni kuwa Molinga si kama nabahatisha,” alisema.

“Baada ya hapo nilifanya ishara nyingine kama ya kuwanyamazisha mashabiki ambao walikuwa wanaongea maneno hayo makali katika mechi iliyopita na nilifanya hivyo hata muda natoka uwanjani kwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo walikuwa wananishangilia lakini niliwapinga kwani haikuwa hongera ya kweli kwangu.

“Bado tumebakiwa na mechi nane za ligi pamoja na nyingine za Kombe la Shirikisho (FA), bado sijakata tamaa hata nikipata muda mchache wa kucheza nataka kuongeza akaunti yangu ya mabao,” alisema.

EYMAEL AMBAKISHA MOLINGA

Eymael alisema ameridhishwa na kiwango cha Molinga na ni miongoni mwa wachezaji ambao amependekeza majina yao kwa msimu ujao.

“Nieleze tu ukweli leo miongoni mwa wachezaji ambao nimependekeza majina yao kwa viongozi na nataka kubaki nao ni Molinga kwa maana hiyo kama atafanya uamuzi wa kuondoka kutokana na ofa ambazo anazo hayo ni yake mwenyewe,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.