Unamtaka Kroos? Utangoja sana aisee

Thursday May 21 2020

 

MADRID, HISPANIA. KAMA unamtaka Toni Kroos basi utangoja sana. Kiungo huyo wa Kijerumani, anayekipiga huko Real Madrid amesema tena kwa kusisitiza hafikirii kuhama ndani ya mwaka huu na atabaki Bernabeu hadi mwisho wa mkataba wake.

Kwa muda mrefu kumekuwa na ripoti kwamba Kroos ni miongoni mwa wachezaji wanaofikiria kuachana na miamba hiyo ya Bernabeu, wakisubiri dirisha la usajili lifunguliwe huku mahali anapotaka kwenda ni kwenye Ligi Kuu England.

Staa huyo wa zamani wa Bayern Munich kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na Manchester United na amekuwa kwenye rada za miamba hiyo ya Old Trafford kwa muda mrefu tangu mwaka 2013 walipokuwa chini ya Kocha David Moyes.

Hata hivyo, kwa miaka hiyo sita, Kroos ameendelea kubaki kwenye kikosi cha Los Blancos huku mpango wake ni kuendelea kuitimikia timu hiyo inayonolewa na Zinedine Zidane hadi mwisho wa mkataba wake 2023.

“Ukweli mpango wangu wa kuihama Real Madrid utakuwa miaka mitatu ijayo. Hapo itakuwa sawa, kwani wakati huo nitakuwa na umri wa miaka 33 na nitajitazama kama naweza kuendelea kubaki,” alisema.

“Kama mambo yatakwenda vizuri, basi itabaki kuwa hivyo katika mpango wa kubaki hapa, mwaka mmoja zaidi na pengine kuendelea zaidi. Sifungi suala la kuhama, lakini kuhusu Ligi Kuu England, inayohitaji kucheza soka la nguvu, kwa umri wa miaka 33 sipati picha itakuwaje.

Advertisement

“Miaka mitatu kwenye soka ni mingi sana na miaka mitatu kwenye kikosi cha Real Madrid ni muda mrefu zaidi.”

Kroos amecheza mechi 33 kwenye kikosi cha Real Madrid msimu huu, akifunga mabao matano na kuasisti mara tisa.

Advertisement