Shabiki aliyefariki akishangilia Taifa Stars azikwa leo

Muktasari:

Rupia alipata mshituko na kuanguka akiwa uwanjani wakati Burundi iliposawazisha bao dhidi ya Tanzania alipopelekwa hospitali ya wilaya ya Temeke alikutwa amekufa.

Dar es Salaam. Shabiki Christopher Rupia aliyefariki uwanjani wakati Taifa Stars ikicheza dhidi ya Burundi Septemba 8, mwaka huu amezikwa leo Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Rupia alipata mshituko na kuanguka akiwa uwanjani wakati Burundi iliposawazisha bao dhidi ya Tanzania alipopelekwa hospitali ya wilaya ya Temeke alikutwa amekufa.

Akizungumza msibani, Katibu Mkuu wa TFF, wilfred Kidao amesema Rupia alikuwa shabiki wa timu ya Taifa na nchi nzima itamuenzi kwa uzalendo wake.

“Tumepoteza mtu muhimu kwenye soka na taifa zima ambaye alikua mzalendo hivyo tunapaswa kumuombea alazwe mahali pema” alisema Kidao.

Familia yake imesema imepoteza nguzo kubwa katika familia na wanamuombea apumzike salama.

Mmoja wa waombolezaji na shabiki wa Taifa Stars, Kariro Kariro amewataka wanamichezo wote kuwa na uzalendo kama ilivyokua kwa mzee Rupia.

“Uzalendo ndio kitu kilichomuongoza mzee wetu na mpaka mauti yanamkuta alikua akilipigania taifa kwa kuishangilia timu yetu hivyo inabidi tuige mema aliyokuwa akifanya na tuyaendeleze,”alisema Kariro

Marehemu Rupia alizaliwa Desemba 26, 1959 na kufariki Septemba 8 mwaka huu na mazishi yamefanyika leo Septemba 11, Ukonga jijini Dar es Salaam