Sahare kuivaa Namungo nusu fainali Kombe la FA

Dar es Salaam. Timu ya Sahare All Stars imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuichapa Ndanda FC kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, jana.

Awali, mchezo huo ulimalizika dakika 90 kwa sare ya bao 1-1.

Mchezo huo ulikuwa wa kasi huku kila timu ikishambulia kwa zamu, lakini hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika zilitoshana nguvu ya kwenda mapumziko bila ya kufungana.

Dakika nne baada ya timu kutoka mapumziko wenyeji Sahare waliandika bao kupitia kwa Kassim Haruna huku Ndanda FC ikisawazisha kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Abdul Hamisi katika dakika ya 53.

Baada ya dakika 90 uamuzi wa mikwaju ya penalti ukaamuliwa ndipo wenyeji wakanufaika na baada ya kufanikiwa kusonga mbele. Mikwaju ya penalti upande wa Ndanda ilipigwa na Abdulrazack Mohamed, Abdul Hamisi, Omary Mponda ambao walifunga huku waliokosa ni Aziz Sibo na Vitalisy Mayanga.

Upande wa Sahare mchezaji Ibrahim Millao alikosa wakati Kassim Haruna, Salimu Pyee, Hussein Zola na Ayoub Mrisho wakikwamisha mipira wavuni.

Kabla ya mchezo huo Sahare iliitoa Njombe Mji kwa kuichapa 1-0 hatua ya 64, huku Ndanda ikiichapa 2-1 Cosmopolitan ilhali katika hatua ya 32, Sahare iliichapa Mtibwa Sugar kwa penalti 2-3 baada ya sare ya bao 1-1 dakika ya 90.

Katika hatua hiyo Ndanda FC iliitoa Dodoma FC kwa kuifunga bao 1-0 na ile ya 16 bora iliisambaratisha Kitayosce FC 3-1 wakati Sahare ikiichapa Panama FC 5-2.

Kwa matokeo hayo, Sahare All Stars itakutana na Namungo FC katika mchezo wa nusu fainali ambayo juzi iliichapa Alliance FC kwa mabao 2-0 katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Sahare inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iko kwenye nafasi ya tisa ikiwa na pointi 22 katika hatari ya kushuka daraja wakati Ndanda FC ya Ligi Kuu iko katika nafasi ya 17 na pointi 35.