Ngoma imepinduka Ligi Kuu Tanzania Bara

Thursday June 04 2020
ngoma pic

NI rasmi sasa Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea na kuendelea kuchezwa kwa utaratibu wa kawaida wa timu kucheza nyumbani na ugenini.

Uamuzi huo ulitangazwa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbasi, Mei 31 siku chache baada ya serikali kutangaza kurejesha shughuli za michezo nchini.

“Serikali imetoa mwongozo wa kufuata katika michezo ya Ligi Kuu za Soka Nchini ambazo zinatarajiwa kuanza Juni Mosi, 2020, hivyo ni muhimu kuzingatia na kwa yeyote atakayekiuka taratibu hizo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Serikali imeridhia ligi zote zilizoruhusiwa kurejea kwa mashabiki watakaotaka kuhudhuria viwanjani waruhusiwe kwa taratibu za kawaida isipokuwa tu kwa mechi zitakazotathminiwa.

Kuhusu mtindo wa uendeshaji wa ligi za soka, Serikali inaruhusu ligi za soka ambazo kikanuni timu inatakiwa kucheza nyumbani na ugenini kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kiafya,” alisema Dk. Abbasi.

Uamuzi huo wa serikali wa kuruhusu ligi kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ni kinyume cha ule uliotangazwa awali na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alisema kuwa ligi hiyo itachezwa kwa kituo ambacho kitakuwa hapa Dar es Salaam.

Advertisement

Ni wazi kwamba uamuzi wa mechi kuchezwa nyumbani na ugenini umepokewa kwa shangwe na kundi kubwa la timu tofauti na ule wa ligi kuchezwa kwa kituo kwani sasa zitakuwa na uhakika wa kupata mapato kutokana na mechi zao za nyumbani.

Zitanufaika na faida ya kuzoea viwanja vya nyumbani lakini pia sapoti ya mashabiki wao.

Lakini kwa upande mwingine, uamuzi wa mechi kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, unaweza kutokuwa habari ya kuvutia kwa vigogo vya soka nchini Simba na Yanga.

Timu hizo mbili, kimahesabu zingepata faida kubwa iwapo mechi zote zilizobaki zingechezwa jijini Dar es Salaam kwani zilikuwa na rekodi nzuri ya kupata ushindi pindi zinapocheza hapa, faida ya kuvizoea viwanja vya Taifa na Uhuru ambavyo vingetumika kwa mechi hizo lakini pia kutotumia gharama kubwa.

Lakini kubwa zaidi ambalo timu hizo mbili kongwe nchini zitaathirika nalo ni kwamba sasa zitalazimika kucheza baadhi ya mechi ugenini nje ya Dar es Salaam ambako ni wazi kwamba zitalazimika kufanya kazi ya ziada kupata ushindi tofauti na iwapo mechi zingechezwa katika kituo cha hapa.

Mwanaspoti inakuletea tathmini ya mechi ambazo zinaziweka Simba na Yanga katika wakati mgumu baada ya uamuzi wa mtindo wa nyumbani na ugenini kuendelea kutangazwa.

SIMBA

Simba imebakiza mechi 10 katika ligi na inaongoza msimamo ikiwa na pointi 71 na inahitaji ushindi katika michezo mitano tu ili itangaze rasmi ubingwa.

Katika mechi ilizobakiza, nne itacheza jijini Dar es Salaam na sita italazimika kwenda ugenini.

Mechi nne ilizobakiza hapa jijini hazionekani kama tishio kubwa kwake kwani itacheza dhidi ya Mbao FC, Alliance, Ruvu Shooting na Mwadui FC ambazo zimekuwa haziwasumbui sana pindi zinapokuja jijini.

Lakini kama isipovuna pointi 12 katika mechi hizo, inaweza kujikuta ikipokonywa tonge mdomoni kwani itakuwa na mechi ngumu za ugenini dhidi ya timu ambazo zinaweza kutibua hesabu zao.

Mbeya City vs Simba

Mechi tano za mwisho ugenini dhidi ya Mbeya City, Simba wamekuwa na matokeo mazuri kwa kuibuka na ushindi mara nne na kupoteza moja.

Hata hivyo, kwa sasa wanakutana na Mbeya City ambayo imekuwa ikifanya vizuri nyumbani ambapo katika mechi tano zilizopita, iliibuka na ushindi mara tatu, kupoteza moja na sare moja.

Ugumu mwingine kwa Simba ni kwamba Mbeya City ipo chini ya Amri Said ambaye anaifahamu vilivyo Simba na amekuwa akiipa wakati mgumu kila timu anayoinoa inapokutana nayo.

Prisons vs Simba

Moja ya timu ambazo zimekuwa zikiisumbua vilivyo Simba pindi inapoenda ugenini nje ya Dar ni Prisons.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika mechi tano zilizopita ambazo zilichezwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Simba imepata ushindi mara mbili, Prisons mara mbili na zimetoka sare mara moja.

Na ikumbukwe kwamba hata mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam msimu huu, timu hizo zilitoka sare tasa.

Ndanda vs Simba

Ndanda haina rekodi nzuri nyumbani dhidi ya Simba kwani tangu iipopanda msimu wa 2014/2015, imecheza na Simba mara tano, ikipoteza nne na kutoka sare moja.

Hata hivyo, ugumu wa pambano la msimu huu unaweza kuchochewa na mambo mawili, kwanza, Ndanda wako katika vita ya kupigania kubaki Ligi Kuu lakini pia wamekuwa tishio nyumbani ambako katika mechi tano zilizopita za ligi, wameshinda tatu na kutoka sare mbili.

Namungo vs Simba

Ushindani ulioonyeshwa na Namungo FC katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ugenini dhidi ya Simba waliopoteza kwa mabao 3-2, unawapa wengi imani kuwa Simba ina kibarua kipevu pindi itakapoenda Uwanja wa Kassim Majaliwa kule Ruangwa, Lindi.

Simba haijawahi kupata ushindi katika uwanja huo na pia Namungo imepoteza mchezo mmoja tu uwanjani hapo katika Ligi Kuu msimu huu.

Coastal vs Simba

Rekodi ya Coastal Union dhidi ya vigogo katika Uwanja wa Mkwakwani ni jambo linaloashiria upinzani mkali ambao Simba itakutana nao pindi itakapoenda hapo msimu huu.

Coastal mbali ya kufanya vizuri nyumbani, msimu huu imeibuka na ushindi hapo dhidi ya Azam na kutoka sare mbele ya Yanga.

Polisi Tanzania vs Simba

Katika mechi tano zilizopita ambazo Polisi walicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, imetoka sare mara tatu na kushinda mbili.

Lakini hata hivyo ushindani wa hali ya juu ambao ilionyesha dhidi ya Simba katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, ni kengele ya hatari kwa vinara hao wa ligi pindi watakapokutana nao.

YANGA

Mabingwa wa kihistoria wa taji la Ligi Kuu, Yanga, wako katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi zao 51 na kama watachanga vyema karata zao katika mechi zilizobakia na watani wao wakateleza, wanaweza kufanya maajabu na kutwaa ubingwa msimu huu.

Yanga wenyewe wamebakiza michezo 11 ambapo kati ya hiyo, mitano watakuwa ugenini na sita nyumbani.

Katika michezo sita ya nyumbani, mechi ambazo zinaonekana zinaweza kuwa ngumu ni mbili dhidi ya Namungo na ile dhidi ya Azam lakini nyingine dhidi ya Mwadui, Singida United, JKT Tanzania na Ndanda haziwapi sana presha.

Hata hivyo, mechi tano za ugenini ambazo Yanga imebakiza ukiondoa ile ya Mwadui, nne zinaonekana hazitokuwa nyepesi na inapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuvuna pointi 12.

Kagera vs Yanga

Kumbukumbu ya mchezo uliopita wa mzunguko wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam, unatoa picha ya wazi ya ushindani ambao Yanga ijiandae kukabiliana nao huko Kagera.

Katika mchezo huo, Yanga ilichapwa mabao 3-0 nyumbani na Kagera Sugar ambayo imekuwa na hulka ya kuvimbia vigogo.

Kana kwamba haitoshi, timu hizo mbili pia zimepangwa kukutana katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Biashara United vs Yanga

Moja ya mechi zinazoiumiza kichwa Yanga bila shaka ni ile ya ugenini dhidi ya Biashara United.

Kwanza hawana historia nzuri mbele ya timu hiyo pindi wanapokutana katika Uwanja wa Karume Musoma, kwani mara moja waliyokutana, Yanga ilipoteza ikiwa ni msimu uliopita.

Ukiondoa hilo, Biashara United wamekuwa tishio nyumbani katika siku za hivi karibuni ambapo wamepata ushindi katika mechi tano mfululizo za mwisho za ligi ambazo wamecheza nyumbani.

Mtibwa Sugar vs Yanga

Mtibwa imekuwa na mwendo wa kusuasua msimu huu lakini huwa na tabia ya kubadilika na kuwa tishio nyumbani pindi ikutanapo na timu kubwa.

Hilo liliweza kujidhihirisha msimu uliopita ambapo licha ya kutofanya vizuri, iliwaduwaza Yanga kwa kuwachapa bao 1-0.

Lipuli vs Yanga

Ndoto za Yanga kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam msimu uliopita zilikatishwa na Lipuli ambayo iliwachapa bao 1-0 katika mechi ya hatua ya nusu fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Samora huko Iringa.

Kana kwamba haitoshi, Lipuli pia iliwachapa Yanga kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita ambao ulichezwa kwenye uwanja huo.

Ugumu wa mechi ambazo Yanga imekuwa ikicheza dhidi ya Lipuli katika Uwanja wa Samora ni wazi kwamba utawafanya waende msimu huu wakiwa na tahadhari kubwa.

Makocha wafunguka

Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck alisema hadhani kwamba ligi kuchezwa kwa utaratibu uliozoeleka kutawaathiri.

“Tumepoteza mechi moja tu nje ya Dar es Salaam msimu huu hivyo, sioni kama kuna tatizo lolote. Tunajiandaa vizuri na tunaamini tunaweza kupata ushindi sehemu yoyote ile tunapokwenda kukutana na adui uwanjani,” alisema Vandenbroeck

Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema kuwa hakuna kinachowapa hofu juu ya uamuzi huo.

“Kabla ya changamoto zilizojitokeza za janga la corona, ligi ilikuwa inachezwa kwa mtindo huo na bila hili jambo, maana yake tungekwenda tu kucheza ugenini.

“Ingeamriwa kuchezwa Dar es Salaam lingekuwa ni jambo jema, lakini bado sio shida kama itabakia kuchezwa nyumbani na ugenini kwani, tumejiandaa kwa ushindani na kikosi kiko tayari kwa ushindani,” alisema Eymael.

Advertisement