Morrison amtolea mlinzi kisu, arudisha pesa za Yanga

STRAIKA kipenzi cha Yanga, Bernard Morrison juzi usiku aliibua sekeseke kwenye kambi ya timu hiyo huku ikidaiwa alimtolea kisu mmoja wa walinzi wa kambi ya timu na vilevile ametema mpunga aliowekewa kwenye akaunti wa usajili.

Tukio hilo linadaiwa kutokea huku Yanga ikiwa na mechi ngumu ya kufuzu nusu fainali ya FA dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa. Licha ya viongozi wa kuchaguliwa pamoja na kocha kugoma kulizungumzia, inadaiwa Morrison alimtolea kisu mlinzi huyo ambaye alimfuata ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa ndani ya Hoteli ya Regency ilipo kambi ya Yanga.

Mmoja wa wachezaji wa Yanga aliyeshuhudia picha hilo kwa dirishani alisema; “Baada ya timu kutoka mazoezini, Morrison alirejea na timu na akaenda kula na wenzake na baada ya chakula ndio filamu ikaanza. Alitoka nje ya eneo la mapokezi na kulifuata gari ndogo ambayo ndani yake ilikuwa na ndugu yake mmoja kati ya wawili anaoishi nao hapa nchini.

“Mmoja wa walinzi wa timu alimfuata pale kwenye gari ili ajue anaongea na nani, lakini baada ya muda alitaka kuondoka na ile gari.

“Akazuiwa akaambiwa haruhusiwi kutoka kwa kuwa hawana taarifa yoyote ya kuondoka kwake, akaanza kutoa lugha chafu kisha akatoa kitu kama kisu. Akamtishia kama anataka kumdhuru yule mlinzi hapo hapo akapata upenyo na kuondoka na hakurudi tena,” alisema huku ikidaiwa usiku huohuo mabosi wa Yanga walionyesha kukerwa na tukio hilo na kumsaka mpaka kwake lakini wakamkosa mpaka aliporudi mida mibovu na Kocha Luc Eymael akamchenjia na kumtoa kwenye orodha ya kikosi cha jana.

Ofisa mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alipoulizwa jana alidai Morrison alisahau viatu vyake nyumbani hivyo alivifuata na ikatokea sintofahamu kidogo wakati anatoka kutokana na ulinzi wa uhakika uliopo kambini hapo. “Kusema aligombana na walinzi sio kweli, ila walipishana kauli tu na walinzi wakati akitoka kwenda kufuata viatu vyake na baadae akarudi,” alisema na kuzikana habari zilizoonekana mitandaoni.

KURUDISHA FEDHA

Habari za ndani ya Yanga zinasema uongozi umemwingizia kiasi cha fedha za mkataba wake mpya wa miaka miwili, lakini akakataa na kuwaambia watu wa benki wazitoe na kuzirudisha kwa mwekaji.

“Kuna pesa zimeingizwa kwenye akaunti yake amewaambia watu wa benki wazitoe hazitambui, inavyoonekana alikuwa hajamalizana na Yanga na sasa ni kama safari yake kutua Simba imeiva,” kilisema chanzo chetu.

Habari zinasema Morrison ameahidiwa donge nono Simba ndiyo maana amegoma kuongeza mkataba Jangwani licha ya kwamba tayari walishakubaliana kila kitu. Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii Instagram, Facebook, Twitter na Mwananchi Digital tutakujuza kitakachoendelea.