Koulibaly vita ya wababe wawili EPL

Friday May 22 2020

 

NAPLES ITALIA. VITA ya kunasa huduma ya beki wa kati wa Napoli, Kalidou Koulibaly imeripotiwa kubaki kwa timu mbili pekee kwa sasa, miamba ya Ligi Kuu England, Manchester United na Liverpool.

Jambo hilo limekuja baada ya mabingwa wa soka wa Ufaransa, matajiri Paris Saint-Germain kuripotiwa kujitoa kwenye mbio za kumnasa Msenegali huyo.

Awali, PSG walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kunasa saini ya Koulibaly, lakini kujitoa kwao kunafanya Liverpool na Man United kubaki wenyewe wenye nguvu kubwa ya kumshawishi beki huyo akaenda kujiunga na timu zao.

Liverpool wanamtaka Koulibaly akacheze sambamba na Virgil van Dijk huko Anfield, wakati Man United wanataka huduma yake akawe pacha wa Harry Maguire kwenye chama la Old Trafford.

Newcastle United nao wanahitaji saini yao, lakini Koulibaly bila ya shaka atahitaji kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Napoli wao wameshakubali yaishe kwamba watapoteza huduma yake kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka huu.

Advertisement

Ripoti mpya zinadai kwamba huduma ya beki huyo kwa sasa inaweza kupatikana kwa Pauni 63 milioni tu baada ya bei yake kushuka kutokana na janga la corona.

Everton, wanaonolewa na kocha wa zamani wa Napoli, Carlo Ancelotti nao wanahitaji saini yake, lakini shida ni kwamba soka la Ulaya linaweza kuwatibulia kwenye mpango wao wa kunasa saini yake. Koulibaly mwenyewe pia amedai hapendelei kabisa na kwenda kucheza kwenye Ligue 1 kwa sababu ligi hiyo imekuwa haina ushindani kabisa.

Advertisement