KMC, Mbao FC patachimbika

Muktasari:

  • KMC inayoshiriki ligi kwa mara ya kwanza msimu huu imekusanya pointi 49 ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo, huku Mbao ikikusanya pointi 44 ikishika nafasi ya 13.

KAZI imeanza mapema, kwani hata kabla KMC na Mbao hazijakutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, klabu hizo zimeanza kuchimbana mkwara kila moja ikitamba kuvuna alama tatu baada ya dakika 90.

Kocha Msaidizi wa KMC, Ahmad Ally alisema wenyeji wao wasitarajie mteremko wa kuvuna pointi tatu kwao kwani hata wao wanazihitaji ili kumaliza kwenye nafasi nzuri katika Ligi Kuu.

KMC inayoshiriki ligi kwa mara ya kwanza msimu huu imekusanya pointi 49 ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo, huku Mbao ikikusanya pointi 44 ikishika nafasi ya 13.

Katika mchezo wa kwanza timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kufungana bao 1-1, lakini kuelekea mchezo wa kesho Jumatano kila timu imepania kutoka na ushindi.

“Hakuna majeruhi yeyote na tunaenda kusaka ushindi, tunafahamu mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Mbao inataka ushindi ila kwa maandalizi yetu yatatupa alama tatu,” alisema Ally huku Kocha Mkuu wa Mbao, Salum Mayanga akisema ushindi kwenye mchezo huo ni muhimu kwao kuwako katika vita ya kupambana kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

“Bado tunahitaji pointi ili kujinasua na janga la kushuka daraja, nimewaandaa wachezaji wangu kisaikolojia kuhakikisha tunavuna pointi tatu na kujiweka katika nafasi nzuri,” alisema Mayanga.