Hawa : Mlenda niliokula India ulikuwa bab’kubwa -2

Muktasari:

Wakati kuku anasema ndio chakula cha kwanza kula baada ya kuruhusiwa kula vyakula vya kawaida hospitali, siku hiyo aliagiza wampikie wali na kuku.

Katika toleo lililopita, Hawa Said maarufu ‘Hawa Nitarejea’ alielezea namna uhusiano wake na Diamond ulipokoma, alivyojitumbukiza kwenye janga la ulevi... SOGA NAYE

Katika kuumwa kwake, Hawa anasema chakula kikubwa alichokuwa anakikosa ni kuku, ugali na matembele. Hata hivyo, anashukuru ugali na mlenda alipokuwa India alianza kuula kwani jirani yao Mtanzania aliyekuwa amebeba matembele ya kukaushwa na unga wa mahindi, hivyo alipokuwa akipika anampa.

Wakati kuku anasema ndio chakula cha kwanza kula baada ya kuruhusiwa kula vyakula vya kawaida hospitali, siku hiyo aliagiza wampikie wali na kuku.

AMSHUKURU DIAMOND

Akizungumzia kuhusu msaada wa Diamond, Hawa anasema ni jambo ambalo hakulitegemea kwani ni mtu ambaye hakuwa na mawasiliano naye kwa muda mrefu.

“Tangu tulivyoachana na Diamond kila mtu aliendelea na maisha yake ikiwemo mimi kuzaa na baadaye kuolewa na mwanaume mwingine,” anasema.

“Lakini ajabu katika wanaume wote niliokuwa na uhusiano nao Diamond ndiye aliyejitokeza kunipa msaada na hii ni baada ya kuniona na kunisikia kwenye vyombo vya habari, kwa hilo namshukuru kwani angeweza kuwasaidia wengine, Mungu amuongezee palipompungikia.”

MALKIA WAKE WA NGUVU NI MAMA YAKE

Anasema, mbali na nyota huyo wa Bongo Fleva, mama yake ndiye kila kitu maishani mwake.

“Mbali na Diamond mama yangu mzazi ndiye mtu aliyekuwa karibu sana na mimi wakati wote, kwa kunipa moyo na kunitaka nizingatie kila ninachoambiwa na madaktari ili niweze kurudi katika hali ya kawaida,” anasema.

“Hivyo ukiachana na Diamond pamoja na vyombo vya habari, mama yangu ni mtu mwema sana kwangu hakunikana kutokana na shida nilizokuwa nazo, alikubaliana na hali yangu akawa karibu nami muda wote.”

Anasema, “nakushukuru mama sina cha kukulipa, Mwenyezi Mungu aendelee kukuongeza pumzi ili niendelee kushuhudia ukuu wako kwangu, wewe ndiye malkia wangu wa nguvu.”

MALENGO YAKE BAADA YA UGONJWA

Hawa anasema baada ya kupona, malengo yake ni kufanya biashara na muziki kwa kuwa anaamini muziki tu bila kuwa na kazi nyingine mbadala ni vigumu kuendesha maisha.

“Kama nilivyosema wakati naumwa kuwa nikipona nataka kufanya biashara, malengo yangu yako palepale, hayajabadilika kwa kuwa naamini ni moja ya njia ya mimi kujiingizia kipato ukizingatia nina mtoto anayehitaji kwenda shule na kumpatia huduma nyingine za kibinadamu kama ilivyo kwa watoto wengine,” anasema Hawa.

AFUNGUKA MADHARA YA POMBE

Hawa anasema katika madhara makubwa aliyoyapata baada ya kutumia pombe ni pamoja na kutumia dawa kwa muda mrefu akifikiri kuwa anaumwa ini wakati ugonjwa uliokuja kutambulika baadaye ni wa moyo.

Madhara mengine, Hawa anasema, ni kupoteza dira ya maisha yake na kusemwa vibaya na watu mambo ambayo yalimuumiza na hatakaa ayasahau na kuwaonya watu kuwa pombe haiwezi kuwa suluhu ya matatizo yanayowasibu.

“Siwezi kutamka kwamba nimeacha pombe lakini kwa kilichonikuta nadhani ni funzo kwangu, nawashauri na kuwaambia Watanzania kitu kinachoitwa pombe si kizuri kwen ye maisha ya kawaida,” anasema.

Hata hivyo ana sema hapo alipofika sasa, hatasahau

mc hango wa

wanahabari, mama yake Ndagina Hassan na Pilli Missanah wa kituo cha kuwahudumia waathirika wa dawa za kulevya kiitwacho Pillimissa kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.

KWANINI AMEIMBA WIMBO WA KUCHEKA

“Nimeuita wimbo wangu ‘Kucheka’ kwa sababu ndio kitu pekee ambacho nilikuwa nakitamani tangu nimeanza kuumwa, sikuwahi kucheka kwani muda wote nilikuwa na maumivu, nilikuwa mtu wa kulia na huzuni.”

Hawa anasema, “nilimisi kucheka, hivyo nimeamua kuachia huu wimbo ukiwa na ujumbe mkubwa kwangu sambamba na kutoa asante kwa Watanzania na ni wimbo ambao nilitumia hela zangu kurekodi kuanzia Audio na video.”

Anasema hata Babu Tale, meneja wa Diamond, hakumshirikisha katika hilo, zaidi ya alipouachia saa 3:00 usiku kwenye Youtube alimfahamisha kuwa auangalie na kutoa maoni yake.

“Baada ya kumwambia Babu Tale vile, nilizima simu na kulala, lakini kesho yake alinipigia simu na kuniambia nijiandae kwenda na mimi kwenye shoo ya Wasafi Dodoma na ndio pale mliponiona nikirudi tena jukwaani nikiwa na Diamond na kuwakumbushia mashabiki kibao cha ‘Nitarejea,” anasema.

AMTAJA RUBBY MAFANIKIO YA MUZIKI

Katika wanamuziki wa kike, Hawa anamtaja Rubby kuwa miongoni mwa wale wanaomkosha.

“Nimefuatilia nyimbo zake anafanya vizuri na ana sauti nzuri, naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza na kumwambia aendelee kupambana, ni msanii mzuri na mkubwa kwa nchi yetu.”

ANATAMANI KUFANYA KAZI NA LAVALAVA

Anasema baada ya kutoka na wimbo wake mpya, kwa sasa ana mpango wa kuimba wimbo wa dini akilenga kumshukuru Mungu kutokana na makuu aliyomfanyia.

“Sijajua ni lini, lakini hili lipo kwenye akili zangu. Pia natamani kufanya kazi na Lava Lava ni msanii ambaye nimefuatilia kazi zake na kubaini kuwa naweza kufanya naye kazi na ikafanya vizuri kutokana na namna anavyoimba tunaendana,” anasema.