JICHO LA MWEWE: ‘Hassan Kessy yupo Zambia, Chama yupo Dar’

RAFIKI mmoja aliyekuwa na hasira alinipigia simu wiki iliyopita. Mjadala wa wachezaji wa kigeni umepamba moto kweli kweli. Aliamua kutoa hasira zake za moyoni kupitia simu yangu. Kuna mjadala kuhusu wachezaji wa kigeni kupunguzwa. Waziri wa upande wetu huu amewaambia wadau wengine wa michezo kujua namna ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni hapa nchini. Unaweza kudhani wachezaji wenyewe ni wengi. Bado ni wachache sana tofauti na kelele zetu.

Hapa ndipo rafiki yangu mmoja kutoka Ilala aliponipigia simu kwa hasira kuu. Mwanzoni nilidhani anaongea kwa masikhara, lakini baadaye nilichambua hoja zake licha ya kwamba alizitolea kwa hasira kali.

“Huyu Waziri atuache. Yaani anaamini kuwa hawa vijana wetu wanazibiwa na wageni? Ahh wapi. Hawa watoto wa siku hizi ni Chips mayai sana. Wamelegea sana. Hawapendi mazoezi. Kazi yao kukaa instagram tu.

“Umewahi kumuona Tshishimbi huko Instagram? Umewahi kumuona Wawa huko Instagram? Halafu hawa wachezaji wa kigeni ni watu wa kazi tu. Sasa sisi watoto wa siku hizi wamelegea sana brother. Tukiondoa wageni tutakuwa na Ligi ya walegevu.” Aliongeza maneno kwa hasira. Nilijaribu kutafakari nikagundua inawezekana. Kuna wachezaji wachache wazawa ambao, wamefikia ukomavu wa akina Wawa na Tshishimbi. Wakati nikiwaza rafiki yangu akaendelea kubwatuka kwa hasira.

“Halafu dunia ni huru hii. Kila mmoja akacheze anakoweza. Kama wao wanakuja kwetu, kwanini sisi tusiende kwao? Ujinga huu. mbona (Hassan) Kessy yuko Zambia na (Clotuos) Chama yuko hapa Tanzania. Kila mmoja na njia yake.”

“Tatizo hawa watoto wetu hawataki kutoka. Wameridhika na hivi vigari vyao Vi-IST basi wanajiona wamemaliza. Juzi nimepishana na mmoja anakaa benchi tu klabuni kwake lakini jinsi alivyofungulia muziki mkubwa katika gari utadhani ndiye Kagere vile”.

Kufikia hapo nikawaza. Hili la kwanza Chama yupo Dar, Kessy yupo Zambia. Ni kweli. Mpira unashangaza sana. Jaribu kuangalia vijana wa Kiingereza wanaotesa soka la Ujerumani. Akina Jadon Sancho. Lakini kuna Wajerumani kibao nao wapo England.

Nikawaza jinsi ambayo kuna Waingereza wanacheza Hispania. Kama vile akina Kieran Trippier. Lakini hapo hapo kuna Wahispaniola kibao wanacheza katika Ligi Kuu ya England. ndivyo maisha ya soka yalivyo. Rafiki yangu hakuishia hapo. Aliendelea kubwatuka maneno makali ambayo mengine siwezi kuyaandika hapa. Hata hivyo, mwisho mwisho aliongea hoja za msingi zaidi.

“Brother Edo, huyu Waziri na watu wake wangejikita zaidi kutenga maeneo ya watoto kucheza. Leo maeneo ya wazi yote yamegeuzwa gereji. Viwanja vya shule navyo vimejengwa madaraja. Zamani wakati wa mapumziko uwanja wa shule ulikuwa unagawanywa mara nane watoto wanacheza soka. Muda wa mapumziko hawaendi nyumbani kula, wanacheza soka. Leo watoto hawana mahala pakucheza halafu tunalalamika wageni?”

“Unapakumbuka pale Jangwani? Kulikuwa na viwanja kama nane hivi. Timu kibao zilikuwa zinafanya mazoezi pale. Kabla ya timu za wakubwa watoto walikuwa wanajiweka fiti pale. Leo wamejenga ofisi za Mabasi. Hakuna kiwanja hata kimoja . Hata Kaunda yenyewe imekufa.”

Naam, hapa alikuwa ameongea ukweli. Vipo wapi viwanj vya wazi? Watoto wetu siku hizi wanakesha katika simu. Hawataki shida. Ndio sababu kijana ana umri mdogo tayari ana presha na kisukari. Ni kweli, kabla ya kutafakari kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni nchini lazima tujiulize. Nadhani ni baada ya viwango vya wazawa kushuka. Kwanini viwango vilianza kushuka? Lazima tupate majibu kutoka kwa wahusika. Wakubwa wasikwepe lawama za soka kushuka na kusingizia wageni. Kuna mahala tumekosea. Inabidi turudi nyuma na kujua tulikosea wapi. Ni kweli ungemchukua mchezaji wa kigeni katika nafasi ya Edibily Jonas Lunyamila? Isingewezekana. Majuzi tumeona mchango wa wachezaji wa kigeni ndani ya Simba ambacho kilifika robo fainali ya michuano ya Afrika. Leo hatuwezi kutumia wachezaji wa ndani tupu kufika nafasi ile. Wachezaji walioisaidia Taifa Stars kufika Afcon ni wale wanaocheza nje. Na hii ina maana kuna mambo mawili lazima tuyafanye. Kwanza ni kurudisha mchezo katika njia zake. Pia, kuwalazimisha wazawa wazuri waliopo nchini wakajaribu bahati zao nje ya mipaka yetu.