Eymael afungiwa miaka miwili, faini Sh8 milioni

Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), imemfungia miaka miwili na faini ya sh 8 milioni kocha wa Yanga, Luc Eymael.
Eymael ametiwa hatiani kwa makosa mawili ikiwemo ubaguzi na udhalilishaji na  tuhuma dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mjumbe wa kamati ya Nidhamu ya TFF, Alex Mushumbusi amesema wameridhika na ushahidi uliotolewa dhidi ya kocha huyo na atanza kutumikia adhabu hiyo kuanzia leo.
Hata hivyo Mushimbuzi amesema Eymael ana haki ya kukata rufaa katika ngazi ya juu ambayo ni Kamati ya Rufaa ya TFF.

"Tulipokea malalamiko kutoka TFF kuhusu kocha wa Yanga, Luc Eymael ambaye alitoa maneno ya kibaguzi , kiudhalilishaji na sio ya kimpira akiishambilia Yanga na TFF."
"Tuliwasiliana na Luc ikiwemo kumtumia hukumu dhidi yake na kumpa wito wa kutakiwa kuhudhuria kikao cha kamati ya nidhamu kilichoketi Agosti Mosi kwenye ofisi za TFF.
"Aliamua kutuandikia kuwa atatuma wawakilishi wake walioko Tunisia hivyo tukajiridhisha kuwa hakuwa na nia ya kuhudhuria  kikao hicho na hivyo kuendelea na kusikiliza ushahudi wa upande wa mashataka."amesema Mushumbusi.
" Tumesikiliza ushahidi na kujiridhisha hivyo kwa kosa la kwanza ambalo ni kutoa maneno ya kibaguzi na udhalilishaji amefungiwa kujihusisha na soka kwa miezi 24 (miaka miwili) na faini ya sh 3 milioni ikiwa ni kwa mujibu wa bara ya 41(13) kanuni ya  udhibiti wa makocha.
"Kosa la pili  ni  kuituhumu TFF kuipendelea Simba, hivyo amepigwa faini ya sh 5 milioni ikiwa ni kwa mujibu wa ibara ya 53(2) ya kanuni za nidhamu za TFF"amesema Mushumbusi.
Mushumbusi amesema  maamuzi dhidi ya kocha huyo pia  yatapelekwa kwenye Shirikisho la Soka Duniani(FIFA).

Eymael anatuhumiwa kufanya kosa hilo baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli ambapo Yanga ilishinda bao 1-0, mechi iliyochezwa Uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Hata hivyo, Yanga baada ya kumfuta kazi, TFF walitoa taarifa ya kumchukulia hatua kali za kinidhamu kocha huyo huku Cham cha Soka Afrika Kusini (SAFA) nao wakitoa taarifa ya kumfungia kocha huyo kujihusisha na mpira wa miguu nchini humo.