Chelsea vs Manchester City acha wauane

LONDON ENGLAND. KWENYE msimamo wa Ligi Kuu England, wapo kwenye nafasi ya nne na pointi zao 51. Mpango wao ni kuhakikisha hawang’oki ndani ya Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Vita ya kufukuzia nafasi kwenye Top Four ni kali, huku nyuma yake kukiwa na Manchester United, Wolves, Tottenham, Sheffield United na pengine Arsenal wote wanafukuzia nafasi hiyo, wakifukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Leo, Alhamisi kuna kasheshe zito huko Stamford Bridge. Frank Lampard na jeshi lake la The Blues atashuka uwanjani kumkaribisha Pep Guardiola na kikosi chake cha Manchester City. Wababe hao wa Etihad wameonyesha kuwa kiboko, kwenye mechi mbili walizocheza tangu Ligi Kuu England iliporejea, wamefunga mabao manane na kuvuna alama zote sita.

Lakini, rekodi za Guardiola dhidi ya Chelsea, ameshinda mechi tano, sare tano na kuchapwa mara nne. Kwa upande wa Lampard, huo utakuwa mchezo wake wa 101 tangu alipoanza kuinoa Chelsea, huku kwenye mechi zake 100 zilizopita, ameshinda 46.

Kwa ujumla wake, Chelsea na Man City zitakutana kwa mara ya 150 kwenye ligi. Chelsea imeshinda 60, imechapwa mara 50 katika mechi 149 zilizopita. Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana Alhamisi, huku mara ya mwisho mchezo huo ulipofanyika Stamford Bridge pia, The Blues walishinda 2-1, Boxing Day 1935.

Man City wao wameshinda mara sita na kupoteza tatu katika mechi tisa za mwisho walicheza kwenye ligi dhidi ya Chelsea. Hata hivyo, Chelsea ndio wanaowatesa zaidi Man City, wakiwafunga mara nyingi zaidi ya timu nyingine zote kwenye Ligi Kuu England, mara 25. Mchezo wao wa mwisho uliopigwa Etihad, Man City ilishinda 2-1, shukrani kwa mabao ya Kevin de Bruyne na Riyad Mahrez, huku lile la kujifariji la Chelsea, lilifungwa na kiungo katili wa mpira N’Golo Kante.

Timu hizo mbili, kila moja imeshawahi kuifunga nyingine 6-0. Chelsea ilifanya hivyo msimu wa 2007/08, wakati Man City ilifanya hivyo 2018/19. Mara ya mwisho, Man City walipokwenda Stamford Bridge, walichapwa 2-0, Kante na David Luiz wakitikisa nyavu.

Ukiweka kando mchezo huo wa Stamford Bridge utakaosubiriwa kwa hamu, mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England itashuhudia mechi nyingine kadhaa zitakazopigwa leo, ambapo Burnley wao watakuwa nyumbani kuwakaribisha Watford.

Arsenal baada ya kuchapwa kwenye mechi mbili zilizopita, watakwenda ugenini kwa Southampton kusaka ushindi wao wa kwanza tangu ligi iliporudi upya, ili kufufua matumaini ya kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao.

Hata hivyo, mechi hiyo ya St Mary’s haitazamiwi kuwa nyepesi kutokana na Southampton kuwa kwenye ubora wao mkubwa kwa siku za karibuni, huku kocha Mikel Arteta akiwa na mapengo kadhaa kwenye kikosi chake kutokana na mastaa wake muhimu akiwamo kipa Bernd Leno kuumia kwenye mechi zilizopita na David Luiz atakuwa nje.