Capello adai Ronaldo amevuruga Madrid

Thursday May 21 2020

 

MILAN, ITALIA. KOCHA, Fabio Capello amefichua kwamba supastaa wa Brazil, Ronaldo amemsababisha matatizo makubwa sana kwenye kikosi cha Real Madrid kutokana na kupenda starehe na kugeuza vyumba vya kubadilishia nguo vya Santiago Bernabeu kuwa baa.

Straika huyo Mbrazili aliyefahamika kwa jina la utani la ‘The Phenomenon’ alikuwa akielekea miaka yake ya mwisho ya soka wakati alipokuwa chini ya Capello kwa kipindi cha miezi sita huko Bernabeu katika msimu wa 2006-07.

Kocha huyo Mtaliano, ambaye alimwelezea Ronaldo kuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa zaidi kuwahi kumnoa, mgogoro wao uliishia kwa Ronaldo kuuzwa kwenda AC Milan, Januari 2007. Kwa wakati huo waliokuwa pamoja, Capello na Ronaldo walikuwa hawaangaliani usoni.

“Mchezaji mwenye kipaji zaidi kuwahi kumnoa alikuwa Ronaldo,” alisema Capello.

“Lakini, alikuwa mchezaji aliyenisababishia matatizo mengi sana. Alikuwa akifanya sherehe kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kutibua kabisa. Kuna siku, Ruud Van Nistelrooy alinifuata na kusema, ‘kocha, vyumba vinanuka pombe tupu.’

“Kisha Ronaldo alienda Milan, tukaanza kushinda, lakini kama nitazungumzia mchezaji aliyekuwa na kipaji kikubwa, bila ya shaka alikuwa Ronaldo.”

Advertisement

Capello baadaye alikuja kusema kwamba licha ya kutibuana huko nyuma, kwa sasa wawili hao wamekuwa wakisalimiana vizuri kabisa kila wanapokutana. Ronaldo alifunga mabao 104 katika mechi 177 alizochezea Real Madrid na kuisaidia timu hiyo kubeba La Liga 2003 na alifunga mabao manne tu katika mechi 13 alizocheza chini ya Capello.

Capello yeye alishinda ubingwa wa ligi msimu huo, lakini alifutwa kazi Juni 2007 na miezi sita baadaye, alichaguliwa kuinoa England.

Advertisement