NYUMA YA PAZIA: Mbappe kwenda Liverpool? Niamsheni usingizini

MELWOOD. Uwanja wa mazoezi wa Liverpool. Kylian Mbappe Lottin anatembea taratibu na Jurgen Klopp. Mkononi ameshika jezi namba 7. Kifuani hii jezi imeandikwa Standard Chartered. Jezi nyekundu ya Liverpool.

Kamera zinamzunguka. Anatabasamu kwa bashasha. Na Klopp naye anatabasamu kwa bashasha. Wanaishika jezi kwa pamoja. Picha nyingi zinapigwa. Dunia inashikwa kwa butwaa. Liverpool wamevunja rekodi ya uhamisho ya dunia. Pauni 240 milioni. Kwa ajili ya Mbappe.

Umewahi kuifikiria picha hii. umewahi kupata mawazo haya. Liverpool wanaota ndoto hii. Na ndio maana naiita ndoto. Haiwezekani. Sioni hili likitokea. Siku hizi imekuwa kawaida kwa mitandao ya England kumuhusisha Mbappe na Liverpool. Kimekuwa kitu cha kawaida.

Sijui habari hizi zinatoka wapi. sijui hata kuna wazo hili. Nianzie wapi? naanza hapa kwamba uhamisho wa Mbappe lazima uvunje rekodi ya uhamisho wa dunia. Lazima iwepo klabu ya kujikamua zaidi ya pauni 230 milioni kumng’oa Mbappe kutoka PSG.

Liverpool wanaweza kutoa pesa hizo? Sidhani. Na hawajahi kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia mahala popote katika rekodi hizo. Timu ya mwisho kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kutoka England ilikuwa ni Manchester United mwaka 2016 waliponunua Paul Pogba Labile kutoka Juventus kwa dau la pauni 90 milioni.

Kabla ya hapo? Newcastle walimnunua Alan Shearer kwa dau la pauni 15 milioni kutoka Blackburn Rovers mwaka 1996. Kabla ya hapo? Sheffield Wednesday walimnunua Jackie Sewell kutoka Notts County mwaka 1951. Walimnunua kwa pauni 34,500

Kadri utakavyorudi nyuma na nyuma hauwezi kuiona Liverpool katika rekodi hizi. Na pesa imepanda thamani zaidi. Liverpool wanaweza kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia? Sidhani kama wanaweza kulipa zaidi ya pauni 200 milioni kwa ajili ya mwili mmoja wa mwanadamu.

Lakini pia wana sababu nyingine. Kama una Sadio Mane, Mohamed Salah na Roberto Firmino, kwanini ulipe pauni 200 milioni kwa ajili ya Mbappe. Liverpool wana mtu ambaye amewageuza akina Mane kuwa Galacticos. Huyu ni Klopp. Kubaki na Klopp ni ushujaa tosha kuliko kumnunua Mbappe.

Klopp anaweza kukutengenezea Mbappe mpya katika kikosi cha Anfield. Kama tu alivyomgeuza Mane kuwa supastaa. Kama alivyomgeuza Salah kuwa Supastaa, na kama alivyomgeuza Firmino kuwa supastaa. Kuna maeneo mawili tu Klopp hakuwa na shida ya kutengeneza mastaa wake akalazimika kuingia sokoni na kutoa pesa nyingi. Pale langoni kwa Allison Becker na pale katika eneo la kati la ulinzi alipoamua kutoa pauni 75 milioni kumnunua Virgil van Dijk.

Vinginevyo sioni akitoa mabilioni ya pesa kwa ajili ya kumnunua mtu katika eneo ambalo alishalitibu kwa muda mrefu sasa. Salah, Mane na Firmino ni utatu utakatifu ambao hauwezi kuukuta popote duniani. Msimu uliopita walitwaa ubingwa wa Ulaya na msimu huu wanatwaa ubingwa wa England. Sidhani hata kama Klopp anamuhitaji Lionel Messi katika timu yake.

Huu ni upande wa Liverpoool. Vipi upande wa Mbappe mwenyewe? Sidhani kama anaitaka Liverpool. Kama moyo unamwambia anaweza kwenda Liverpool basi ni kwa ajili ya kuigeuza Liverpool kama kituo cha mwisho kabla ya kwenda Santiago Bernabeu.

Mbappe anaonekana wazi kuwa mchezaji wa Real Madrid. Mbappe ndiye Galactico anayefuatia katika soka letu baada ya Messi, Cristiano Ronaldo na Neymar. Na inawezekana kwa sasa anasimama juu ya Neymar katika mpangilio wa Magalacticos.

Wachezaji wa kariba yake wameumbwa kwenda Hispania. Ni rahisi kuwaza Mane kwenda Real Madrid kuliko kuwaza Mbappe kwenda Liverpool. Barcelona na Real Madrid ni kilele cha wachezaji wote duniani ambao makali yake yanaishangaza dunia.

Mbappe anaiwaza Real Madrid. Zaidi ya hili ni kwamba wote wanawazana. Yeye mwenyewe hawezi kuogopa kwenda Real Madrid kwa sasa kwa sababu hakuna watu wa kumtisha pale mbele. Namba yake anaiona. Ufalme wake anauona. Kama Ronaldo angekuwepo angeweza kuogopa kuishi katika kivuli chake. Kama tu Neymar alivyoogopa kivuli cha Messi.

Lakini, Mbappe anaenda Santiago kuwa mfalme licha ya kuwa na umri wa miaka 21 tu. Hana muda wa kupoteza. Ronaldo angekuwepo wangemwambia achelewechelewe kwanza mpaka Ronaldo aondoke. Hapo ndipo angeweza kuwaza kujizungusha kwenda Liverpool. Lakini kwa hali ilivyo sasa, ahofie nini?

Hata hivyo, upande wa pili pia Madrid nao wanamuhitaji Mbappe. Kwanza kabisa Ronaldo aliondoka na Eden Hazard amesuasua kuziba pengo. Amekwenda akiwa na uzito mkubwa na mpaka sasa hajazikonga nyoyo za Madridista.

Achilia mbali pengo la Ronaldo lakini pia Real Madrid inabidi isukwe upya kwa mara nyingine. Ile timu yao ambayo ilitwaa ubingwa wa Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo inaonekana imegota. Umri wa wengi mle umetoweka. Kuanzia kwa Karim Benzema, Toni Kroos, Luka Modric, Marcelo na wengineo.

Madrid inabidi iundwe upya. Lakini hapo hapo kumbuka muasisi wa kuvunja rekodi za uhamisho katika karne hii, Florentino Perez bado hajatoa onyo lolote kwa dunia tangu alipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 2013 wakati alipomnunua Gareth Bale kutoka Tottenham.

Labda kwa sababu ya corona anaweza kurudisha pochi lake mfukoni, lakini vinginevyo ni yeye tu ndiye ambaye kwa sasa anaweza kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kando ya Manchester City ambao wana pesa za mafuta.

Nahisi Perez atataka kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kwa Mbappe kwa sababu ni Galactico mkubwa zaidi kwa sasa.

Wote wawili wanataka kwa sasa. Siioni nafasi ya Liverpool. Ndoto ya kumuona Klopp akitembea na Mbappe katika nyasi za Melwood au Anfield nadhani itabakia kuwa ndoto.

Sijui uzushi huu wa Mbappe kwenda Liverpool unatokea wapi?