Wananitaka! Gundogan afunguka kuhusu Manchester United

Sunday February 28 2021
gundogan pic

MANCHESTER, ENGLAND

NDO hivyo. Ilkay Gundogan amefichua ni kweli Manchester United ilikuwa timu ya kwanza kutaka kumleta kwenye Ligi Kuu England miaka kadhaa kabla ya kusaini dili la kuchezea mahasimu wao, Manchester City.

Kiungo huyo Mjerumani, Gundogan yupo kwenye kiwango bora kabisa kwa soka lake kwa sasa, akifunga mabao 11 katika mechi 19 za ligi na hiyo ilikuwa kabla ya mchezo wa jana Jumamosi dhidi ya West Ham United.

Ubora wake ndani ya uwanja, unamfanya Gundogan kuwa mmoja wa wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu kwenye Ligi Kuu England, huku chama lake la Man City likionekana kabisa kwenda kushinda ubingwa wa tatu hilo kwa mara ya tatu katika kipindi cha misimu minne.

Huu ni msimu wa tano kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 tangu alipotua England, akikipiga huko Etihad alikonaswa akitokea Borussia Dortmund mwaka 2016.

Gundogan alisema mambo yangekuwa tofauti kama angekwenda kukipiga kwenye kikosi cha Man United.

Advertisement

Kwa muda mrefu, Mashetani Wekundu wa Old Trafford waliripotiwa kumtaka kiungo huyo kwa kipindi alichokuwa akiwasha moto kwenye Bundesliga.

Mchezaji mwenyewe alipoulizwa kuhusu madai hayo Man United wamemtaka, Gundogan aliambia: “Ni ukweli mtupu.

“Kulikuwa na mazungumzo. Nadhani ilikuwa miaka miwili au mitatu hivi kabla sijajiunga na Man City, kipindi hicho nilikuwa naitumikia Borussia Dortmund.

“Mmoja wa wachezaji wenzangu kipindi hicho, Shinji Kagawa, alisajiliwa na United na kuna mtu aliniambia, walikuja mara kadhaa kwenye mechi zetu kumtazama anavyocheza kabla ya kumsajili.

“Kisha wakaanza kunivutia, lakini mazungumzo hayakuendelea zaidi ya hapo kwa sababu Borussia Dortmund waliwaambia wazi hawana mpango wa kuniuza.

“Nami nilikuwa bado nina miaka kadhaa kwenye mkataba wangu, hivyo sikuwa na uwezo wa kusema chochote kwa kipindi kile. Hivyo, mwisho ya yote, uhamisho haukutokea.”

Kagawa alinaswa na Man United kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2012, huku Gundogan alibaki kwenye kikosi cha Dortmund na kukisaidia kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka uliofuatia.

Mambo hayakwenda sawa kwa Kagawa huko Man United, huku Gundogan mwenyewe akidai hana anachojutia kutokana na mambo yalivyo kwenda na kushindwa kukamilisha dili la kwenda kukipiga Old Trafford.

Alisema: “Nina furaha kwa sababu mwisho wa yote nilijiunga na Man City. Naamini kila kitu kinatokea kwa sababu. Kama kuna kitu chochote nitataka kukibadilisha kwa maisha yangu, sina. Najivunia na mahali hapa na nafurahia wakati wangu wa kuwa hapa.

“Mwisho ya wote, tumezoea kuishi kwenye maisha haya ya kushindana. Nawakubali sana Man United kwa kile ambacho wamekuwa wakifanya na nimekuwa nafurahia kucheza dhidi yao, nafurahia kuwa nao kwenye jiji moja na hivyo ndivyo soka lilivyo.”

Advertisement