Saini zao pesa ndefu

LONDON, ENGLAND

HII ni rasmi. Kylian Mbappe ndiye mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa, huku mshangao mkubwa ukiibuka kwamba, Erling Haaland hayupo hata kwenye 10 bora ya mastaa wa thamani kubwa.

Staa wa Paris Saint-Germain, Mbappe, 22, yupo kwenye kiwango matata kabisa kinachompeleka kwenda kuwa mchezaji bora zaidi duniani.

Mbappe hivi karibuni aliwafanya vibaya Barcelona baada ya kufunga hat-trick kuisaidia PSG kushinda 4-1 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika Nou Camp.

Na kwa mujibu wa KPMG’s Football Benchmark, Mbappe - ambaye tayari ameshashinda ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa 2018, ndiye mwanasoka wa thamani ya juu zaidi duniani kwa sasa. Staa huyo anatajwa kuwa na thamani ya Pauni 159 milioni, licha ya mtikisiko wa kiuchumi unaosababishwa na janga la virusi vya corona.

Jambo hilo limemfanya Mbappe kuwa na thamani ya zaidi ya Pauni 50 milioni zaidi ya wachezaji wengine.

Mbappe amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda Real Madrid kuunda Galacticos mpya miezi michache ijayo. Los Blancos wanataka kunasa huduma ya staa huyo wa PSG, ambaye utoto wake wote amekuwa akiishabikia miamba hiyo ya La Liga na huenda akatua Bernabeu kwenye dirisha lijalo la usajili.

Na matumaini ya Real Madrid kwamba Mbappe atakwenda kutengeneza pacha na Haaland itakapofika 2022, ambapo miamba hiyo ya Bernabeu wanaamini watamalizana na Borussia Dortmund itakapofika mwakani, ambapo straika Haaland atakuwa anapatikana kwa Pauni 63 milioni.

Lakini, Haaland, 20, ambaye pia yupo kwenye rada za Chelsea na Manchester United, anashika namba 11 kwenye orodha ya wanasoka wenye thamani kubwa duniani, licha ya kiwango chake matata kabisa ndani ya uwanja na mkali huyo wa kimataifa wa Norway, anathamanishwa kuwa na thamani ya Pauni 95 milioni.

Viwango hivyo vya thamani ni habari njema kwa England, ambapo kuna mastaa wake watano wa kikosi cha Three Lions wameingia kwenye 10 bora ya mastaa wenye thamani kubwa sokoni.

Straika Harry Kane na winga Raheem Sterling wamelingana, kila mmoja akiwa na thamani ya Pauni 108 milioni, wakati Jadon Sancho - staa mwingine anayesakwa na Man United, anashika namba nne kwa kuwa na thamani ya Pauni 101 milioni.

Marcus Rashford amelingana na Neymar na Mohamed Salah, wakiripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 99 milioni kwa kila mmoja, huku mkali wa Manchester City, Kevin De Bruyne akitajwa kuwa na thamani ya Pauni 98 milioni na wakali wawili wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold na Sadio Mane wakitajwa kuwa na thamani ya Pauni 95 milioni kila mmoja.

Mastaa wengineo wanaokipiga kwenye Ligi Kuu England, Bruno Fernandes anashika namba 12 kwa kuwa na thamani ya Pauni 92 milioni, huku mastaa wa Chelsea, Kai Havertz (Pauni 77 milioni) na Timo Werner (Pauni 76 milioni) wakishika nafasi ya 19 na 20.