Wamecheza mechi kibao za kimataifa bila kupoteza

LONDON, ENGLAND. HISPANIA ilivunja rekodi ya Italia ya kutofungwa mechi za kimataifa wakati ilipowachapa kwenye nusu fainali ya michuano ya Uefa Nations League wiki iliyopita.

Italia ilikuwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mechi 37, lakini ilikuja kutibuliwa na vijana wa Luis Enrique walipokubali kipigo cha mabao 2-1.

Katika mchezo huo, La Roja ilifunga mabao yake yote mawili kupitia kwa Ferran Torres, wakati lile la Azzurri lilifungwa na Lorenzo Pellegrini.

Italia ya kocha Roberto Mancini ilipoteza mechi yake ya kwanza baada ya mechi kibao.

Hizi hapa timu za taifa ambazo ziliweka rekodi ya kucheza mechi kuanzia mechi 30 bila kupoteza.


Italia mechi 37 (2018 - 2021)

Mbio za Italia kutopoteza mechi 37 za kimataifa ilianza tangu mwaka 2018, Italia ilipocheza na Ukraine na kuambulia sare ya bao 1-1 chini ya kocha anayeinoa timu hiyo Mancini.

Italia ilifuzu michuano ya Euro 2020 kwa rekodi ya asilimia 100 chini ya Mancini ambaye aliwahi pia kuinoa Manchester City mwaka 2008. Michuano ya Euro ilipoanza , Italia walikuwa walikuwa wababe na kushinda mechi zote za hatua ya makundi ikishinda dhidi ya Uturuki, Uswisi na Wales kabla ya kuing’oa Ubelgiji na Austria hatua ya mtoano.

Italia waliendelea hivyo na kuiondosha Hispania kwa changamoto ya mikwaju ya penalti kwenye mchezo wa nusu fainali na fainali ilipomeyana na England na kubeba ubingwa.

Vijana hao wa Azzurri waliweka rekodi ya Euro ya kutofungwa mechi 11 mfululizo kabla ya kuruhusu bao golini mwao ilipomenyana na Austria hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Licha ya mechi nyingi ambazo walishinda Italia ilipata sare ilipomenyana dhidi ya Bulgaria na Uswisi kabala kurejea tena na kuichapa Lithuania 5-0.

Italia iliendelea hivyo hadi kufika jumla ya mechi 37 bila ya kufungwa, sare saba ambazo iliambulia na kufunga mabao 93 wakir uhusu mabao 12 ya kufungwa kabla ya Hispania kuvunja rekodi yao.


Hispania – mechi 35 (2007 -2009)

Ushindi dhidi ya England wa bao 1-0 mwaka 2007 ilionyesha matumaini ya Hispania.

Andres Iniesta alifunga bao lake kwa mara ya kwanza akitokea benchi kwenye mtanange huo uliochezwa Uwanja wa Old Trafford. Kipindi hicho Hispania ilisheheni mastaa wakali kama Iker Casillas, Sergio Ramos, Carles Puyol, David Silva, Cesc Fabregas na Fernando Torres. Rekodi yao ya kutofungwa mechi 30 ilianza na michuano ya Euro ambayo ilifanyika mwaka 2008 wakiendelea hivyo hadi mechi za kufuzu Kombe la Dunia ilipoanza kutimua vumbi mwaka 2010.

Rekodi ya Hispania ilivunjika mwaka 2009 baada ya kufungwa mabao 2-0 ilipocheza na Marekani kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Lakini mambo mazuri yalianza kuja baada ya kipigo hicho Hispania ikiweka rekodi ya kutofungwa michezo 27 katika mechi 28 ambazo Hispania ilicheza, ambapo mwaka 2010 na 2012 ulikuwa wa mafanikio kwa Hispania kwani ilibeba ndoo ya Kombe la Dunia na Euro.


Brazil - mechi 35 (1993 - 1996)

Brazil ilicheza michezo 35 bila ya kufungwa rekodi ambayo hadi bado inakumbukwa na magwiji wa soka nchini humo kuanzia mwaka 1993 baadaye kuvunjwa 1996.

Rekodi hiyo ilijumuishwa na michuano ya Kombe la Dunia ambayo Brazil ilibeba kuanzia mwaka 1994.


Argentina – mechi 31 (1991 - 1993)

Argentina ilianza mbio hizo baada ya kufungwa na Ujerumani Magharibi kwenye fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990.

Argentina iliamka na kuonyesha kiwango bora kuanzia mwaka 1991 kwa kutoruhusu kufungwa jumla ya mechi 31 kabla ya kuvunjwa mwaka 1993.

Ndani ya miaka hiyo miwili Argentina ilibeba taji la Copa America, kipindi hicho Gabriel Batistuta akiwa kinara wa mabao wa Argentina wa muda wote kabla ya Lionel Messi kuvunja rekodi yake.


Ufaransa – mechi 30 (1994 - 1996)

Ufaransa ilikaribia rekodi ya Argentina kabla ya kuvunjwa mwaka 1996 na Czech Republic kwenye nufu fainali ya michuani ya Euro kwa mikwaju ya penalti. Ufaransa ikaendeleza vipigo kwa kufungwa bao 1-0 kwenye mechi ya kirafiki ilipomenyana na Denmark, lakini ikaja kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia miaka miwili baadaye kabla ya michuano ya Euro kuanza mwaka 2000.

Kwa upande wa Ufaransa mbio hizo zilianza na ushindi wa bao 1-0 ilipomenyana na Italia 1994, huku magwiji wa soka Zinedine Zidane na Lilian Thuram wakicheza mechi hiyo kwa mara ya kwanza.