Ngoma imenoga Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- Hapa chini kuna uchambuzi, rekodi na mambo muhimu ya kufahamu kwa kila mechi ya robo fainali ya michuano hiyo.
NEW YORK, MAREKANI: MICHUANO ya Kombe la Dunia kwa klabu inayoendelea huko Marekani imefikia patamu ambapo sasa zimebakia timu nane zinazopambana kuanzia leo kutafuta tiketi ya kwenda nusu fainali kutoka robo fainali.
Hapa chini kuna uchambuzi, rekodi na mambo muhimu ya kufahamu kwa kila mechi ya robo fainali ya michuano hiyo.
Robo fainali ya kwanza itakuwa kati ya Fluminense na Al-Hilal mchezo ambao utakuwa unazikutanisha timu hizo kwa mara ya kwanza.
Al-Hilal imejizolea sifa tele baada ya kuichapa Manchester City mabao 4-3 katika hatua ya 16 bora licha ya ubora wa timu hiyo.
Hata hivyo, wapinzani wao Fluminense pia walifika hatua hiyo baada ya kuindoa Inter Milan kwa kuichapa mabao 2-0 katika 16 bora.
Timu itakayopita katika mechi hii itakutana na mshindi kati ya Palmeiras na Chelsea. Mchezo huu utapigwa leo saa 4:00 usiku.
Palmeiras ambayo ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi A, ikishinda mechi moja na kutoka sare mbili kisha katika hatua ya 16 bora, iliichapa Botafogo kwa bao 1-0 baada ya muda wa ziada, itakutana na Chelsea kwenye robo fainali.
Mchezo huu unaonekana kuwa unaweza kuwa wa kisasi kwa Palmeiras ambao walipoteza katika mchezo wa fainali ya michuano hii mwaka 2022 kwa mabao 2-0.
Licha ya ubora wake, Palmeiras inakabiliwa na changamoto ya kuwakosa wachezaji muhimu wawili ambao ni nahodha Gustavo Gomez ambaye anatumikia adhabu ya kadi za njano mbili alizoonyeshwa katika mechi tofauti, pia beki wa kushoto Joaquin Piquerez atakosekana kutokana na adhabu.
Wapinzani wao Chelsea, walianza kwa kupoteza 3-1 dhidi ya Flamengo, lakini walijirekebisha kwa kushinda mechi tatu mfululizo, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 4-1 katika 16 bora dhidi ya Benfica.
Hata hivyo, matajiri hawa wa London pia watawakosa wachezaji wao muhimu akiwamo kiungo Moises Caicedo atakayekosekana kutokana na kadi ya njano, lakini watapata ahueni kwa urejeo wa mshambuliaji wao Nicolas Jackson. Mchezo huu utapigwa katika dimba la Camping World, Orlando.
Upande mwingine vigogo wa Ulaya, wamekutanishwa wenyewe kwa wenyewe, PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya watakutana na mabinga watetezi wa Bundesliga, Bayern Munich kesho kuanzia saa 1:00 usiku.
Mchezo huu ambao utapigwa kwenye dimba la Mercedes-Benz, Atlanta mshindi atakutana na mbabe wa mechi kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund ambayo pia inasubiriwa kwa hamu kwa sababu itawakutanisha ndugu wawili, Jude na Jobe Bellingham. Mechi ya Madrid na Dortmund itapigwa MetLife Stadium, saa 5:00 usiku.