Kisa dili, Gyokeres aacha mchumba wake

Muktasari:
- Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Ureno, TV Guia, wapenzi hao waliachana kabla ya Gyokeres kwenda likizo Ugiriki.
LISBON, URENO: INAELEZWA straika wa Sporting Lisbon anayewindwa na Arsenal na Manchester United, Viktor Gyokeres ameachana na mpenzi wake raia wa Ureno, Ines Aguiar, hivi karibuni na sababu ikitajwa kuwa ni masuala ya usajili.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Ureno, TV Guia, wapenzi hao waliachana kabla ya Gyokeres kwenda likizo Ugiriki.
Uvumi ulianza kuenea kuhusu kuachana kwao baada ya Aguiar kutoonekana kwenye harusi ya mchezaji mwenzake wa Sporting, Morten Hjulmand na Emilie Sofie Nissen, ambaye anaripotiwa kuwa rafiki wa karibu na Aguiar.
Muigizaji huyo alienda likizo kwenye kisiwa cha Formentera, Hispania, huku Gyokeres yeye akielekea Mykonos, Ugiriki.
TV Guia imeripoti kuwa Gyokeres alimjulisha Aguiar uamuzi wake wa kuachana naye kabla ya kuanza likizo ambapo chanzo cha karibu na mshambuliaji huyo raia wa Sweden kinaeleza kuwa Gyokeres hataki kitu chochote kimfungamanishe na Ureno, hasa kwa kuwa tayari ameamua hatobaki Sporting msimu ujao na inaelezwa mpenzi wake huyo alikuwa mzito kuondoka Ureno.
Gyokeres anadaiwa kumweleza Aguiar msimamo wake, ambapo licha ya mrembo huyo kukubali alionekana kuwa amesikitika sana, kwani anaripotiwa kumpenda sana mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26.
Hadi sasa sio Gyokeres wala Aguiar ambaye ametamka hadharani kuhusu taarifa hizo za kuachana, ingawa bado wanafuatana kwenye mitandao ya kijamii.
Habari hizi za kuachana zimekuja katikati ya sakata kali la uhamisho kati ya Gyokeres na Sporting Lisbon msimu huu wa joto.
Mshambuliaji huyo amehusishwa kwa kiasi kikubwa na kuondoka katika timu hiyo licha ya kutokuwa katika maelewano mazuri na mabosi wa Sporting.
Ripoti zinasema kuwa Gyokeres hatarudi Sporting, kwani amekerwa na kauli zilizotolewa na rais wa timu hiyo, Frederico Varandas, licha ya Gyokeres kupewa wiki moja zaidi ya mapumziko.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden amekasirishwa na hatua ya mabingwa hao wa Ureno kushindwa kutimiza makubaliano ya awali ya kumruhusu kuondoka kwa bei ya chini tofauti na iliyoandikwa kaitka kifungu chake.
Varandas alisema: “Sporting iko tulivu juu ya suala hili. Pili, Sporting haina haja ya kumuuza Viktor Gyokeres. Kwa bahati nzuri, tumeshapita zama za kuuza wachezaji wetu tegemeo.”