Wakali waliopiga Hat-Trick wakitokea benchi Ligi Kuu England

LONDON ENGLAND. SUPASTAA, Son Heung-min alihitaji dakika 27 tu za kuwa ndani ya uwanja kufunga mabao matatu wakati Tottenham Hotspur iliposhusha kipigo kizito kwa Leicester City katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Son alifunga hat-trick akitokea benchi na jambo hilo linamfanya kuingia kwenye orodha ya mastaa wa kibabe kabisa waliowahi kutupia nyavuni mara tatu na zaidi baada ya kutokea benchi kwenye mechi za Ligi Kuu England.
Kwenye Ligi Kuu England, kufunga hat-trick ni tukio la kushangilia, lakini kufunga mara tatu baada ya kutokea benchi hilo ni jambo lenye kuvutia zaidi.
Ndani ya Ligi Kuu England zimefungwa hat-trick zaidi ya 200 kwenye historia yake ya miaka 30, lakini sehemu kubwa ya hat-trick hizo zimefungwa na wachezaji ambao wamekuwa wakianzishwa kwenye mechi. Kuna hat-trick chache sana zilifungwa na wachezaji walioingia kutokea benchi na Son wa Spurs anakuwa mchezaji wa saba kufanya hiyo kwenye Ligi Kuu England.
Orodha kamili ya masupastaa waliopiga hat-trick Ligi Kuu England wakitokea benchi hii hapa.
Ole Gunnar Solskjaer (Nottingham Forest 1-8 Man United, Februari 6, 1999)
Akiwa na kumbukumbu za kudumu Manchester United kwa kile kilichotokea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Ole Gunnar Solskjaer alikuwa moto pia kwenye ligi, ambapo Februari 1999 aliandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutokea benchi na kufunga hat-trick kwenye Ligi Kuu England. Wakati Solskjaer anaingia, Man United tayari ilikuwa mbele kwa mabao 4-1 na hiyo ilikuwa dakika 72, Sir Alex Ferguson alipomwingiza ‘muuaji mwenye sura ya kitoto’ ambaye alifunga mabao manne Man United ikiichapa Nottingham Forest 8-1 kwao.
Jimmy Floyd Hasselbaink (Chelsea 5-2 Wolves, Machi 27, 2004)
Miaka mitano baadaye, Jimmy Floyd Hasselbaink alisherehekea miaka yake 32 ya kuzaliwa kwa kuipigia hat-trick Chelsea akitokea benchi kuichapa Wolves 5-2 uwanjani Stamford Bridge. Chelsea ilikuwa kwenye msako wa kuifukuzia Arsenal, ambapo msimu huo ilikuwa moto kwelikweli ikicheza msimu wote bila ya kupoteza kwenye ligi. Hasselbaink wakati anaingia, ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka 2-2, lakini akapigia bao la tatu The Blues katika dakika 77, kabla ya kuongeza jingine dakika 10 baadaye na kukamilisha bao lake la tatu kwenye dakika za majeruhi, The Blues ikishinda 5-2.
Robert Earnshaw (Charlton 1-4 West Brom, Machi 19, 2005)
Robert Earnshaw kwenye ubora wake alifunga hat-trick akitokea benchi kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Charlton wakati huo akiwa zake West Brom. Kipute hicho kilipigwa The Valley, Machi 19, 2005. Katika mchezo huo, Charlton ilikuwa pungufu kwa wachezaji 10 karibu kipindi chote cha kwanza kabla ya Earnshaw hajaingia kufanya jambo la kukumbuka maisha yao yote, ambapo alipiga mabao yake matatu kuifanya West Brom kushinda 4-1. Staa huyo alifunga bao lake la tatu katika dakika ya 89 kwa mkwaju wa penalti.
Emmanuel Adebayor (Derby 2-6 Arsenal, Aprili 28, 2008)
Katika msimu wa 2007/08, Emmanuel Adebayor alikuwa na wakati mzuri sana kwenye kufunga mabao, ambapo alitikisa nyavu mara 30 katika michuano yote, huku akipiga hat-trick dhidi ya Derby uwanjani Pride Park wakati huo akiwa Arsenal. Mashabiki wa Derby walikuwa kwenye wakati mgumu sana mbele ya Adebayor, kwa sababu staa huyo wa Togo aliwapiga pia hat-trick katika mechi ya kwanza ya ligi msimu huo, iliyofanyika Emirates na Arsenal kushinda 5-0. Hat-trick yake ya pili, Adebayor alifunga akitokea benchi na aliwafanya hivyo Derby wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, Pride Park.
Romelu Lukaku (West Brom 5-5 Man United, Mei 19, 2013)
Mechi ya mwisho ya Kocha Sir Alex Ferguon kwenye kikosi cha Man United kabla ya kustaafu alishuhudia mabao 10 kwenye Ligi Kuu England na kuingia kwenye historia ya kipekee, huku ikishuhudia straika Romelu Lukaku akifanya mambo makubwa kipindi hicho akiwa na West Brom. Lukaku alifunga bao dakika tano tu tangu alipoingia kutokea benchi katika kipindi cha pili, kisha alifunga tena mara mbili katika dakika 15 za mwisho wakati West Brom ilipotokea nyuma kwa mabao 5-2 kupata sare ya mabao 5-5 dhidi ya Man United iliyochukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huo.
Steven Naismith (Everton 3-1 Chelsea, Septemba 12, 2015)
Tumekuwa tukisikia mara nyingi kuhusu wachezaji kutumia nafasi. Hakika hilo lilifanywa vyema na Steven Naismith, wakati alipoifanya Everton kuwa bora dhidi ya Chelsea huko uwanjani Goodison Park, Septemba 12, 2015. Naismith alitokea benchi kwenye dakika ya tisa tu, akiingia kuchukua nafasi ya Muhamed Besic, aliyekuwa ameumia na hapo hakumwaangusha kocha wake Roberto Martinez kwa kutupia nyavuni mara tatu, akifunga mabao yote ya Everton kwenye mchezo huo wa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Chelsea.
Son Heung-min (Tottenham 6-2 Leicester, Septemba 17, 2022)
Baada ya kufunga mabao 23 msimu wa 2021/22 na kushea Kiatu cha Dhahabu na Mohamed Salah, Son Heung-min alikuwa hajafunga bao lolote tangu msimu huu wa 2022/23. Staa huyo wa Korea Kusini hakuwa amefunga bao lolote kwenye mechi nane za mwanzo za Spurs kwenye michuano yote. Jambo hilo lilimfanya Kocha Antonio Conte kumwaanzishia benchi dhidi ya Leicester City na jambo hilo lilileta bahati kwa Son. Akiingia dakika 59, Son alifunga bao kuifanya Spurs kuongoza 4-2 na dakika 14 baadaye alikamilisha hat-trick yake kusaidia Spurs kushinda 6-2.