Ronaldo ashambuliwa kutohudhuria mazishi ya Jota

Muktasari:
- Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno na mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi alikuwa anatarajiwa kusafiri hadi Gondomar karibu na Porto kutoa heshima zake za mwisho pamoja na wachezaji wenzake wa klabu na timu ya taifa katika ibada ya maombolezo jana na misa ya mazishi leo asubuhi.
PORTO, URENO: Kutokuwepo kwa Cristiano Ronaldo kwenye mazishi ya pamoja ya nyota wa Liverpool, Diogo Jota na mdogo wake Andre Silva kumesababisha mshangao mkubwa nchini Ureno, leo.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno na mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi alikuwa anatarajiwa kusafiri hadi Gondomar karibu na Porto kutoa heshima zake za mwisho pamoja na wachezaji wenzake wa klabu na timu ya taifa katika ibada ya maombolezo jana na misa ya mazishi leo asubuhi.
Lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 40 hakuonekana kwenye matukio yote hayo — huku gazeti maarufu la Majorca likiripoti kuwa alikuwa likizo visiwani humo na alionekana katika maeneo mawili ya kifahari akiwa kwenye boti ya kifahari yenye thamani ya Pauni 5.5 milioni.
Wachezaji wa Liverpool, Bernardo Silva wa Manchester City na Diogo Dalot wa Manchester United - wote wakichezea timu ya taifa ya Ureno walikuwa miongoni mwa wachezaji waliofika kanisani leo asubuhi — katika Kanisa la Igreja Matriz de Gondomar.
Wachezaji wengine wa Ureno, Joao Cancelo na Ruben Neves walioonekana wakilia usiku wa Ijumaa kabla ya mechi ya Klabu BIna ya Dunia uko Orlando, Marekani pia walifika kanisani kwa wakati pamoja na kocha wa timu ya taifa, Roberto Martinez, ambaye alikuwa Marekani kama sehemu ya kamati ya benchi la ufundi la mashindano hayo - naye alikuwepo.
Mwandishi wa habari wa Ureno, Antonio Ribeiro Cristovao alisema muda mfupi kabla ya misa ya leo kuanza: “Yeye (Ronaldo) ndiye nahodha wa kikosi cha Ureno. Wengi walitarajia angehudhuria. Diogo Jota alikuwa sehemu ya timu. Labda kuna sababu hatuzijui. Kama hatahudhuria, anapaswa kueleza sababu. Ana jukumu hilo. Yeye ni nahodha.”
Mwanahabari wa michezo Luis Cristovao alielezea suala la kutokuwepo kwa Ronaldo akisema ni "haielezeki kirahisi” na kuongeza kuwa: “Kwa kuwa haieleweki, hata sababu yoyote atakayotoa haitakubalika.”
Mchambuzi wa runinga, Pedro Fatela alielezea kuhusu kutokuwepo kwa mshambuliaji huyo wa Al-Nassr akisem: “Kutokuwepo huku kutajadiliwa sana. Lazima kuwe na sababu zitakazotolewa katika siku chache zijazo. Tutajua kwa nini Cristiano hakuweza kusafiri hadi Gondomar kuwa sehemu ya tukio hili. Yeye ni nahodha wote tulitarajia kama makocha na wachezaji walivyokuwepo naye awe bega kwa bega na wenzake.”
Suala hilo limeibua hasira za mashabiki na Wareno wengi ambao wamemshambulia Ronaldo mitandaoni miongoni mwao wakidai ni mtu mbinafsi asiyejali maisha ya wenzake na kwamba hastahili kuheshimiwa. Hata hivyo, mchezaji huyo bado hajibu chochote kutokuwepo kwake kwenye tukio hilo.