Partey apewa kesi ya kubaka

Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Ghana anatuhumiwa pia kufanya unyanyasaji wa mwanamke mwingine wa tatu.
LONDON, ENGLAND: ALIYEKUWA kiungo wa Arsenal, Thomas Partey amefunguliwa mashtaka matano ya madai ya ubakaji yakihusisha wanawake wawili.
Staa huyo wa kimataifa wa Ghana anatuhumiwa pia kufanya unyanyasaji wa mwanamke mwingine wa tatu.
Partey, 32, alidaiwa kufanya makosa hayo kati ya 2021 na 2022, kwa mujibu wa taarifa ya polisi.
Atafikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi huko Westminster, Agosti 5.
Hilo limekuja wakati Partey mkataba wake kwenye kikosi cha Arsenal ukifika kikomo tangu Juni 30 na hakusaini dili jipya, hivyo kwa sasa ni mchezaji huru.
Tuhuma hizo zinazomkabili Partey zinahusisha wanawake watatu tofauti. Anatuhumiwa kufanya makosa matatu ya ubakaji dhidi ya mwanamke mmoja na mawili dhidi ya mwanamke mwingine.
Partey pia ana shtaka jingine linalomkabili la kumfanyia unyanyasaji mwanamke wa tatu.
Wakili wa utetezi, Jenny Wiltshire alisema: “Thomas Partey amekana tuhuma zote hizo.
“Alitoa ushirikiano mzuri kwa polisi katika kipindi chote cha uchunguzi kwa miaka yote. Sasa anakaribisha wakati wa kusafisha jina lake. Kwenye hilo sasa, kesi itaanza kusikilizwa kwenye mahakama za kisheria na mteja wangu hana cha kuzungumza zaidi ya hicho.”
Uchunguzi ulianza kufanyika Februari 2022 baada ya maofisa wa polisi kupokea ripoti ya kubaka.
Ofisa upepelezi, Andy Furphy, ambaye anaongoza jopo la wapepelezi alisema: “Kipaumbele chetu ni kutoa sapoti kwa wanawake ambao wameamua kujitokeza mbele.”
Partey alikuwa kwenye kikosi cha Arsenal kwa miaka mitano tangu aliponaswa mwaka 2020 akitokea Atletico Madrid, ambako alishinda taji la Europa League. Aliichezea nchi yake ya Ghana kwenye fainali tatu za Afcon na Kombe la Dunia 2022.