Vita ya taji la tano kwa Curry, Lebron NBA

Muktasari:
- Stephen Curry, kwa upande wake msimu ukianza atakuwa ameingia wa 16 kucheza mashindano hayo tangu alipochaguliwa na Golden State Warriors 2009 na ameshinda nayo mataji manne.
LEBRON James msimu mpya ukianza Oktoba, mwaka huu atakuwa anacheza Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) kwa msimu wa 22 mfululizo ambapo katika misimu hiyo amechukua taji mara nne akiwa na timu tatu tofauti.
Stephen Curry, kwa upande wake msimu ukianza atakuwa ameingia wa 16 kucheza mashindano hayo tangu alipochaguliwa na Golden State Warriors 2009 na ameshinda nayo mataji manne.
LeBron aliingia NBA 2003 alipochaguliwa katika droo kama namba moja na Cleveland Cavaliers aliyoitumikia mara mbili ambako aliondoka bila kubeba taji awamu ya kwanza, akaenda kuchukua mawili akiwa na Miami Heat kabla hajarudi Cavaliers aliyoipeleka fainali nne mfululizo kuanzia 2015-2018 na kuchukua taji 2016.
Baada ya hapo alihamia Los Angeles Lakers 2019 na hakusubiri kuchukua taji lake la nne akiwa hapo 2020, lakini sasa anataka taji la tano akiwa Lakers ambapo ametajwa kusisitiza kwa mabosi wake waongeze nguvu ya kikosi baada ya kusaini kubaki akilenga taji.
Chef Curry kwa upande mwingine amesema kubaki kwake kwa kuongeza mkataba wiki iliyopita kunalenga taji la tano kwake ndani ya timu hiyo na analitarajia msimu ujao kama ilivyo kwa LeBron na Lakers.