Arsenal wanawake yatwaa Uefa

Muktasari:
- Nyota wa timu ya taifa ya wanawake ya Sweden, Stina Blackstenius, alizima ndoto za Barcelona kutwaa taji lao la tatu mfululizo kwa kuifungia Arsenal bao la ushindi na kuiwezesha kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kumaliza msimu bila ya kushinda taji lolote kwa upande wa wanaume, mashabiki wa Arsenal huenda wakajifuta machozi baada ya timu yao ya wanawake kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Nyota wa timu ya taifa ya wanawake ya Sweden, Stina Blackstenius, alizima ndoto za Barcelona kutwaa taji lao la tatu mfululizo kwa kuifungia Arsenal bao la ushindi na kuiwezesha kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18.
Mshambuliaji huyo, anayejulikana kwa uwezo wake wa kufunga mabao ya ushindi katika michuano mikubwa, alifunga bao hilo muhimu katika dakika ya 75 kwenye Uwanja wa Sporting Lisbon, Ureno, na kuipa Arsenal ushindi wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2007 na hili lilikuwa bao lake jingine muhimu msimu huu, baada ya kufunga la ushindi kwenye fainali ya Kombe la Ligi ya Wanawake.
Katika mechi hiyo ya kusisimua, Arsenal ilifunga bao lililokataliwa baada ya Irene Paredes kujifunga, lakini VAR ikaonyesha kuwa Frida Maanum alikuwa ameotea.
Hata hivyo, licha ya mashabiki 38,356 wengi wao wakiwa ni wa Barcelona kuwazomea, Arsenal walidhibiti mchezo kwa ustadi mkubwa.
Barcelona, ambao wametawala soka la wanawake barani Ulaya kwa miaka ya hivi karibuni kwa kutwaa mataji matatu kati ya manne ya mwisho, walionekana kuzidiwa.
Hata hivyo, kabla ya fainali hiyo Barca iliwahi kukutana na Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Wanawake mwaka 2021 ambapo iliichapa 4-0 na msimu huu imeziondoa timu mbili za England Man City na Chelsea.
Mechi hiyo iliruhudhuriwa na melejendi na viongozi mbalimbali wa Arsenal.