Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Turufu ya Mzize na Dube kwa Jean Ahoua

AHOUA Pict

Muktasari:

  • Moja ya eneo ambalo sasa limekuwa gumzo na mijadala kwenye vijiwe vya kahawa hususani vile vya Simba na Yanga ni mchuano baina ya wafungaji bora, huku Clement Mzize wa Yanga akiwa mzawa peke mwenye moto wa aina yake.

USHINDANI wa mastaa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu umezidi kukolea na kusababisha mambo kuzidi kunoga. Lakini kuna kuna linakwenda kutokea kati ya wachezaji watatu mahiri kwenye mashindano hayo ambao wote wanacheza kwa watani wa jadi.

Moja ya eneo ambalo sasa limekuwa gumzo na mijadala kwenye vijiwe vya kahawa hususani vile vya Simba na Yanga ni mchuano baina ya wafungaji bora, huku Clement Mzize wa Yanga akiwa mzawa peke mwenye moto wa aina yake.

Kama ni karata tungeita turufu. Iko hivi. Moja ya jambo analoombea kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua ni kutolingana na mchezaji yeyote katika idadi ya mabao ya Ligi Kuu kwa msimu huu, kwani nyota huyo kwa sasa kanuni zinambana, licha ya kuongoza vita ya ufungaji.

Ahoua aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Stella Club Adjame ya Ivory Coast, ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao Ligi Kuu Bara akifunga 15, akifuatiwa na Prince Dube na Clement Mzize wote wa Yanga ambao kila mmoja amefunga 13.

Licha ya Ahoua kuongoza vita hiyo, lakini ikiwa mwisho wa msimu ikitokea amelingana idadi ya mabao na mchezaji mwingine, kanuni za Ligi Kuu Tanzania toleo la 2024 zitambana kutokana na nyota huyo kufunga mabao sita ya penalti kati ya 15.

Kanuni ya (13.1) ya Ligi Kuu kuhusu tuzo ya mfungaji bora, inasema mabao yatakayofungwa kwa njia ya kawaida yatakuwa na pointi mbili (2), huku yatakayofungwa kwa penalti yatapewa pointi moja (1), hivyo mwenye pointi nyingi atakuwa mshindi.

Kama itatokea watalingana basi itatumika kanuni ya 13.2, ambayo itatoa nafasi kwa aliyecheza muda mchache zaidi kuibuka mshindi na ikishindikana pia kwa vigezo hivyo, itatumika kanuni ya 13.3 ya mchezaji aliyefunga mabao mengi ugenini.

Kwa mantiki hiyo, mabao ya Ahoua yanampa pointi 24, baada ya kufunga sita ya penalti na tisa ya kawaida, huku kwa upande wa Mzize na Dube ambao wote wamefunga mabao 13 hadi sasa tena bila ya penalti wanaongoza wakiwa na pointi 26 kila mmoja.

Mshambuliaji wa Simba, Leonel Ateba anafuatia kwa kufunga mabao 12, ambapo amekusanya pointi 18, kutokana na mabao sita kati ya hayo ameyafunga kwa penalti.

Nyota wa Simba, Steven Mukwala aliyefunga mabao 11, amekusanya pointi 22 kwani mshambuliaji huyo raia wa Uganda mabao yote aliyofunga hakuna la penalti.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah aliyejiunga na timu hiyo dirisha dogo msimu huu akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, amefunga mabao 11, ambapo kati ya hayo saba ameyafunga kawaida, huku manne yakiwa ni ya penalti.

Nyota huyo wa zamani wa Medeama ya Ghana, licha ya kujiunga na timu hiyo kwa muda mchache, lakini ameonyesha kiwango bora hadi sasa na kuzivutia klabu mbalimbali kuhitaji saini yake, ambapo kutokana na mabao yake amekusanya pointi 18.

Mshambuliaji, Elvis Rupia anayecheza pia Singida Black Stars, amefunga mabao 10 na yote ni ya kawaida jambo linalomfanya kukusanya pointi 20, ingawa kati ya penalti nane ilizopata timu hiyo msimu huu, imekosa mbili ambazo zote alikosa Mkenya huyo.

Sababu za maboresho ya kanuni ya pointi mbili kwa bao la kawaida na moja kwa litakalofungwa kwa penalti, ni kutokana na malalamiko yaliyotokea msimu wa 2022-2023, kwa nyota, Fiston Mayele na Saidi Ntibazonkiza 'Saido' kulingana mabao.

Msimu huo wa 2022-2023, aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele alifunga mabao 17, sawa na kiungo wa zamani wa Simba na Geita Gold, Mrundi Saidi Ntibazonkiza 'Saido' hali iliyosababisha kufanyika kwa maboresho ya kanuni.

Kanuni ya ufungaji bora, ilifanyiwa maboresho kutokana na malalamiko ya mashabiki wengi kuamini, Mayele alistahili tuzo hiyo kwa sababu alifunga mabao machache ya penalti, tofauti na ilivyokuwa kwa 'Saido' aliyefunga mengi msimu huo husika.

Nini maoni yako kuhusiana na mchuano huu. Tuandikie; 0658-376 417.