Vieira aonja ushindi EPL, Palace ikiichapa Spurs

NYOTA wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira ambaye kwa sasa ni kocha wa Crystal Palace ameiongoza timu yake  kuibuka na ushindi wake wa  kwanza  kwenye London derby dhidi ya Tottenham.

Vieira  mwenye asili ya Afrika, aliuanza msimu huu wa EPL kwa kuvuna pointi mbili kwenye michezo mitatu iliyopita.

Mzaliwa huyo wa Senegal aliimaliza Spurs baada ya kuwa pungufu kwa kufanya mabadiliko kadhaa, ikiwemo kumtoa Christian Benteke na kumpa nafasi mshambuliaji wake mpya, Odsonne Édouard.

Spurs iliwabidi kucheza pungufu kuanzia dakika ya 58 kufuatia kwa beki wao, Japhet Tanganga kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambana na nyekundu baada ya kumchezea faulo, Mghana Jordan Ayew.

Kitendo cha Spurs kuwa pungufu kiliwafanya kuzidiwa na vijana wa Vieira huku wakionekana kujilinda zaidi, dakika ya 75 Crystal Palace walipata bao la kuingoza lililofungwa na Wilfred Zaha kwa mkwaju wa penalti uliosababishwa Ben Davies kushika mpira uliopigwa na  Conor Gallagher.

Baada ya Palace kuwa mbele kwa bao hilo, ndipo Vieira alipompa nafasi  Édouard aliyesajili kutoka Celtic.

Hesabu za Vieira zilijipa ndani ya sekunde 28, jamaa akatupia bao la pili na  Palace na dakika ya 90+3 alipiga msumari wa pili kwake na watatu kwa chama lake ambalo limeibuka na ushindi wa mabao 3-0 likiwa nyumbani.