Vanja kiumbe aliyebadili maisha ya Luka Modric

Muktasari:
- Kiumbe huyo ndiye alichora ramani nzima ya Modric kujiunga na miamba hiyo ya Hispania chini ya Rais Florentino Perez, mmoja wa watu ambao kila mchezaji angefurahi kuketi naye katika meza ya mazungumzo na kukamilisha dili.
FUNDI wa mpira, Luka Modric, 39, ameagwa na Real Madrid msimu uliomalizika baada ya kuichezea timu hiyo kwa miaka 13 akishinda mataji yote makubwa na tuzo za hadhi ya juu, ila nyuma ya mafanikio hayo kuna kiumbe anaitwa Vanja Bosnic.
Kiumbe huyo ndiye alichora ramani nzima ya Modric kujiunga na miamba hiyo ya Hispania chini ya Rais Florentino Perez, mmoja wa watu ambao kila mchezaji angefurahi kuketi naye katika meza ya mazungumzo na kukamilisha dili.
Modric, Mchezaji Bora wa Fifa 2018, kabla ya kukutana na Vanja, 43, alikuwa mwanasoka asiye na rekodi yoyote ya kujivunia lakini walipokubaliana kufanya kazi pamoja meza ikapinduka na sasa kuna mengi ya kuzungumza kuhusu kiungo huyo.
Je, kiumbe huyo ni nani na kafanya nini katika maisha ya Modric? Vanja alizaliwa Julai 18, 1982 huko Zagreb ambao ni mji mkuu wa Croatia. Baba yake, Milan Bosnic, alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu na pia aliwahi kumiliki mgahawa katika mji mdogo wa Kutina.
Ikumbukwe alipozaliwa mrembo huyo yaani Zagreb, ni takribani maili 187 kutoka Zadar alikozaliwa Modric hapo Septemba 9, 1985, na hivyo Vanja ni mkubwa kwa Modric akimzidi miaka minne.

Mama yake Vanja, Vanka Bosnic licha ya kusomea uchumi alijishughulisha na kazi za nyumbani alijitahidi kumlea vizuri binti yake huyo lakini baadaye alifanya kazi katika sekta ya elimu.
Hata hivyo, wazazi wake walitalikiana wakati Vanja akiwa na umri wa miaka 11, hivyo akaamua kuishi na mama yake katika nyumba ya babu na bibi yake upande wa mama kwa muda fulani.
Kwa mujibu wa kitabu cha Modric, My Game (2021), mama yake Vanja alilazimika kufanya kazi katika shule ya sekondari iliyokuwa karibu yao ili kumlipia binti yake ada kabla ya kupata kazi huko Zagreb ambako waliweza kupanga nyumba yao wenyewe.
Kuachana kwa wazazi wake kulimfanya Vanja kukulia katika mazingira magumu kwa sehemu ila akajifunza kuwajibika mapema kwa kufanya kazi za nyumbani - majukumu ambayo yamemjenga kuwa mwanamke imara na mwenye mafanikio hadi sasa.
Baada ya kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Zagreb aliposomea uchumi na biashara, Vanja alianza kazi katika shirika la Mamic Sports Agency - shirika maarufu la masoko ya michezo na wachezaji nchini Croatia.

Hapo ndipo alipokutana na Modric 2007, wakati huo nyota huyo alikuwa akichezea Klabu ya Dinamo Zagreb ya huko kwao Croatia ambayo alijiunga nayo 2003 na kuondoka 2008 akitolewa kwa mkopo.
Punde tu, uhusiano wao wa kikazi uligeuka kuwa wa kimapenzi na baada ya miaka minne ya uchumba walifunga ndoa Mei 2010 katika sherehe ya faragha iliyofanyika Zagreb, na mwaka mmoja baadaye walifunga ndoa ya kidini kanisani.
Kipindi wanaoana, tayari Modric alishatua katika Ligi Kuu England (EPL) akiichezea Tottenham Hotspur, na mchezaji mwenzake wa zamani wa Tottenham na timu ya taifa ya Croatia, Vedran Corluka ndiye alikuwa msimamizi (best man) wa harusi yao.
Mtoto wao wa kwanza ambaye ni wa kiume, Ivano, alizaliwa wiki tatu tu baada ya ndoa yao na baadaye walijaliwa kupata mabinti wawili, Ema (2013) na Sofia (2017) ambao mara kadhaa wameonekana uwanjani na baba yao.

Miezi michache baada ya ndoa, Vanja aliacha kazi katika shirika hilo la michezo na kuwa wakala binafsi wa Modric, na yeye ndiye alisimamia mchakato wa uhamisho wa mchezaji huyo kwenda Real Madrid mwaka 2012 akitokea Tottenham.
Vanja alihusika moja kwa moja katika majadiliano ya mkataba wa Modric kwenda Real Madrid - timu iliyompa mafanikio makubwa akishinda mataji manne ya Ligi Kuu Hispania (La Liga) na sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL).
Kubwa zaidi ni kushinda tuzo ya Mchezaji Bora Duniani ya Ballon d’Or 2018 akiwa ni mchezaji wa kwanza kufanya hivyo tangu 2007 ambapo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo walikuwa wanapokezana kuibeba tuzo hizo.

Baada ya uhamisho huo mkubwa, Vanja aliamua kustaafu kazi ya uwakala ili kujikita katika kulea familia yao, huku mtindo wake wa maisha ukipishana na wenza wa mastaa wengi wa soka duniani.
Ingawa Modric ni maarufu duniani, Vanja amejizuia kuwa kwenye mitandao ya kijamii na hupendelea maisha ya faragha. Picha za familia yao huonekana mara chache kwenye ukurasa wa Instagram wa Modric tu. Hata hivyo, licha ya Vanja kuwa mbali na vyombo vya habari na mitandao, ameendelea kuwa nguzo muhimu nyuma ya mafanikio ya Modric akiwa amechangia mengi mazuri katika maisha yake ya soka na kifamilia yao kwa ujumla.