Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zubaa uchekwe!

LIGI Pict

UNAIJUA furaha ya kufanikisha jambo dakika za mwisho huku kila mmoja akikutolea macho kuona kama utafanikiwa au la? Basi jambo hilo hadi kufikia saa 12 jioni Jumapili hii mbivu na mbichi zitafahamika.


Katika muda huo kuna baadhi ya timu na wachezaji binafsi wanafukuzia jambo ambapo katika kipindi hiki cha mwishoni mwa ligi, ukizubaa utachekwa wakati mwenzako akitimiza malengo.


Hiyo ni katika Ligi Kuu Bara pale ambapo raundi ya 30 itakapotamatika kwa kuchezwa mechi nane zenye maana kubwa. Ndani ya saa mbili baada ya saa 10 jioni kila kitu kitakuwa hadharani.



KenGold na Kagera Sugar shughuli yao imeisha mapema kwani ndiyo timu mbili zilizoshuka daraja moja kwa moja, lakini kuna mambo mengine ya kuangaliwa. Fountain Gate yenye pointi 29, hesabu zinaiweka timu hiyo katika nafasi moja ya kucheza mechi za mtoano (play off) ya kuepuka kushuka daraja.

Juu yake kuna Tanzania Prisons (30) na Namungo (32), huku Pamba Jiji (33) kwao ni nafuu kidogo kutokana na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kuwabeba dhidi ya Tanzania Prisons. Ili Tanzania Prisons imalize juu ya Pamba Jiji, inatakiwa kuifunga Singida Black Stars mabao ya kutosha kuondoa tofauti ya mabao baina yao ambayo ni tisa, kisha Pamba Jiji itakapokuwa nyumbani ipoteza kwa KMC.

Katika mechi za raundi ya 30, licha ya kwamba kuna baadhi ya timu hazina presha yoyote kutokana na kutokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja wala kuwania ubingwa, lakini zinapambania nafasi nzuri kwani kuna pesa zinatolewa na mdhamini mwenye haki za matangazo. Kwa mujibu wa mkataba wa Azam Media mgao wa nafasi kuanzia msimu wa 2021-2024, kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya mwisho hazitoki patupu, kwani kuna mgao. Bingwa anapata Sh500 milioni, nafasi ya pili Sh250 milioni, nafasi ya tatu Sh225 milioni, nafasi ya nne Sh200 milioni, nafasi ya tano Sh65 milioni, nafasi ya sita Sh60 milioni, nafasi ya saba Sh55 milioni, nafasi ya nane Sh50 milioni, nafasi ya tisa Sh45 milioni, nafasi ya kumi Sh40 milioni, nafasi ya 11 Sh35 milioni, nafasi ya 12 Sh30 milioni, nafasi ya 13 Sh25 milioni, nafasi ya 14 Sh20 milioni, nafasi ya 15 na 16 Sh10 milioni.


YANGA VS DODOMA JIJI

Mabingwa watetezi, Yanga watakuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kuwakaribisha Dodoma Jiji ambayo imeshajitoa kwenye presha ya kuangukia mtoano.

Yanga yenye rekodi nzuri mbele ya Dodoma Jiji, mchezo huu unaweza kuwachongea barabara nzuri ya kwenda kutetea ubingwa kwani ikishinda itafikisha pointi 79, huku ikihitaji sare pekee dhidi ya Simba kuwa mabingwa. Ubora wa kikosi cha Yanga uliifanya timu hiyo kushinda mabao 4-0 katika duru la kwanza dhidi ya Dodoma Jiji. Katika mechi tisa za ligi timu hizo kukutana, Yanga imeshinda nane na sare moja.


SIMBA VS KAGERA SUGAR

Dimba la KMC Complex jijini Dar, limebeba hatma ya Simba kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ikipambana kuishusha Yanga kileleni. Simba yenye pointi 75 inaikaribisha Kagera Sugar iliyoshuka daraja hivyo inakamilisha ratiba.

Simba ina kumbukumbu nzuri ya kuichapa Kagera Sugar mabao 5-2 katika mchezo wa duru la kwanza, lakini kocha msaidizi wa kikosi hicho, Seleman Matola amesema lazima wapambane kwani aina timu wanayokwenda kucheza nayo ni hatari kutokana na sasa haina cha kupoteza huku wao wakiwa na hesabu kali za ubingwa.

Matola amesema: “Tuko vizuri, tumejiandaa kwa ajili ya mchezo wa kesho (leo) na tunajua tunakutana na timu ambayo ishashuka daraja, siku zote nasema unapokutna na timu ya aina hiyo inakupa wakati mgumu kwani wachezaji wakiwa kwenye hatua hii wanacheza kwa kujionyesha wenyewe.

“Kwa hiyo itakuwa mechi ya ushindani na ngumu lakini sisi tumejipanga pamoja na ugumu wao tupate pointi tatu katika mchezo wa kesho.”

Matola alibainisha kuwa katika mchezo huo kuna uwezekano mkubwa wa kubadili kikosi kutoka kilichocheza dhidi ya KenGold ugenini na kushinda 5-0 ili kutoa nafasi ya kuwapumzisha kwani baada ya hapo wanakwenda kumalizana na Yanga, Juni 25.

“Ndani ya takribani wiki moja tuna mechi tatu (dhidi ya KenGold iliyopita, Kagera Sugar itachezwa leo na Yanga itafanyika Juni 25), kwa hiyo huwezi kuwatumia wachezaji walewale.

“Katika mechi zilizobaki lazima tufanye rotation (mabadiliko ya kikosi), kwa hiyo tutegemee mechi ya kesho (leo) kuwepo rotation,” alisisitiza Matola.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Idd Simba, alisema: “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wa kesho (leo), tunajua Simba ni moja ya timu kubwa lakini na sisi tumejiandaa vizuri kuonyesha upinzania.

“Ndio hatujafikia malengo yetu msimu huu, lakini mechi ya kesho (leo) tutaitumia kumaliza kwa heshima.

“Mechi hizi za mwisho tunazitumia pia kuwachezesha vijana wetu wa chini ya miaka 20 ikiwa ni maandalizi kuelekea Championship, hivyo tunakwenda kucheza sio kwamba hatuna cha kutafuta, tunacho ambacho ni kujiandaa na Championship, kwa hiyo lazima tucheze kwa ushindani.”


MASHUJAA VS JKT TANZANIA

Ni mechi inayozikutanisha timu za jeshi, itafanyika kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma. Zote hazina presha ya kushuka, zinasaka nafasi bora kwa sasa ambapo JKT Tanzania ni ya sita na pointi 35, chini yake kuna Mashujaa yenye pointi 34 nafasi ya saba. Wenyeji Mashujaa watataka kushinda ili kuwa juu na kupata mgao mzuri wa fedha. Duru la kwanza timu hizi zilitoka 0-0.

Kocha msaidizi wa Mashujaa, Charles Fred, alisema: “Maandalizi yapo vizuri, tumejiandaa kwa ajili ya kushinda ili kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea kumaliza nafasi ya tano ya msimamo.”


PAMBA JIJI VS KMC

Kwenye Dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, wenyeji Pamba Jiji wanataka kumaliza ligi kibabe baada ya kushuhudia wenzao KenGold waliopanda pamoja wakirudi Championship, lakini pia kukaa juu ya KMC kutokana na sasa kupishana pointi moja pekee kwenye nafasi ya 10 na 11.

Mbali na kuhitaji kuwa juu zaidi, lakini pia kulipa kiasi cha kupoteza mechi ya duru la kwanza ilipofungwa 1-0 na KMC.

Kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix Minziro, alisema: “Tunawashukuru sana Wanamwanza kwa hamasa yao kwani tumefika hapa kwa ajili yao, nitumie nafasi hii kuwaalika kesho waje kwa wingi kuhitimisha msimu kwa kishindo.”


NAMUNGO VS KENGOLD

Kitendo cha kutoka suluhu dhidi ya Kagera Sugar mechi iliyopita ikiwa nyumbani, kimeifanya Namungo kubaki kwenye mtego wa kuangukia playoff, hivyo leo inahitaji ushindi wa namna yoyote ile kujiweka salama itakapoikaribisha KenGold kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi.

Duru la kwanza, KenGold iliyoshuka daraja ikiwa nyumbani ilipoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Namungo, mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Kocha Msaidizi wa Namungo, Ngawina Ngawina, alisema kilichotokea mchezo uliopita kimekuwa funzo kwao kuelekea kuikabili KenGold, hivyo hawatarajii makosa hayo yajirudie.


SINGIDA BLACK STARS VS TANZANIA PRISONS

Wenyeji Singida Black Stars watakuwa Uwanja wa Liti mkoani Singida kuikaribisha Tanzania Prisons iliyopo kwenye presha ya kuangukia play off.

Singida Black Stars kwa pointi 56 ilizonazo, matokeo ya aina yoyote hayaweza kubadili kitu kwani itaendelea kusalia nafasi ya nne huku ikiwa tayari na tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Tanzania Prisons baada ya mechi iliyopita kupoteza nyumbani kwa mabao 5-0 dhidi ya Yanga, ina mtihani mwingine kwa Singida Black Stars. Duru la kwanza Tanzania Prisons ilifungwa 2-0.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah alisema wanakwenda kupambana ugenini kuona wanamaliza vipi msimu huku wakiamini bado wanayo nafasi ya kuepuka kuangukia play off.


COASTAL UNION VS TABORA UNITED

Mechi ambayo haina presha kubwa kutokana na kila mmoja kujihakikishia msimu ujao atashiriki tena ligi, lakini sasa malengo ni kumaliza kwa heshima.

Wenyeji Coastal Union wakiwa kwenye Dimba la Mkwakwani, wametoka kuichapa Fountain Gate hivyo wanataka kuendeleza mwendo huo mzuri na kumaliza nafasi ya juu zaidi kutoka na nane iliyopo.

Tabora United haijashinda mechi sita mfululizo za ligi zilizopita, hivyo ina mtihani mkubwa leo. Duru la kwanza zilitoka sare ya bao 1-1.


FOUNTAIN GATE VS AZAM

Baada ya kuwa tayari inafahamu itacheza playoff, Fountain Gate inaikaribisha Azam ambayo nayo imejihakikishia nafasi ya tatu. Timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, huku duru la kwanza Azam ikishinda 2-0.


CLEAN SHEET

Mbali na vita ya nafasi kwa kila timu, pia kuna kuwania kumaliza na clean sheet nyingi ambapo kwa sasa kipa wa Simba, Moussa Camara anaongoza akiwa nazo 18, anahitaji moja tu kujihakikishia ufalme wake kwani amemuacha Djigui Diarra (Yanga) aliyekusanya 16.

Msimu uliopita, aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi alimaliza kinara wa clean sheet akiwa nazo 15, akifuatiwa Djigui Diarra (Yanga) aliyemaliza na 14.


UFUNGAJI BORA

Hapa kuna vita ya wachezaji wa Simba na Yanga, kwa mbali Singida Black Stars. Kwa sasa kinara wa mabao ni Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 16, akifuatiwa na Lionel Ateba (Simba), Clement Mzize na Prince Dube wanaocheza Yanga ambapo wote hao watatu wamefunga mabao 13.  Chini yao kuna Steven Mukwala wa Simba (12), Jonathan Sowah wa Singida Black Stars (12), Pacome Zouzoua wa Yanga (11) na Gibril Sillah wa Azam (11).