Mo Salah, Bruno wagombea tuzo

Muktasari:
- Salah na Mac Allister ni miongoni mwa mastaa sita wakaochuana kuwania tuzo hiyo baada ya kuisaidia Liverpool kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England. Wachezaji wengine ni Bruno Fernandes, Alexander Isak, Cole Palmer na Declan Rice - ambapo watachuana kuwania tuzo hiyo itakayotolewa Agosti mwaka huu.
LONDON, ENGLAND: MOHAMED Salah na Alexis Mac Allister wapo kwenye mchakamchaka wa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Kulipwa huko England baada ya kuwa na msimu bora lakini mashabiki wa Liverpool wanashangazwa na kitendo cha beki Virgil van Dijk kuondolewa kwenye kinyang’anyiro.
Salah na Mac Allister ni miongoni mwa mastaa sita wakaochuana kuwania tuzo hiyo baada ya kuisaidia Liverpool kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England. Wachezaji wengine ni Bruno Fernandes, Alexander Isak, Cole Palmer na Declan Rice - ambapo watachuana kuwania tuzo hiyo itakayotolewa Agosti mwaka huu.
Mashabiki wa Liverpool walishangazwa na kitendo cha Van Dijk kuondolewa kwenye mchakato huo.
Shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii: “Van Dijk hayupo ni ajabu. Kiwango cha juu kabisa,” wakati mwingine aliongeza: “Hii orodha, hebu niambieni inakuwaje Bruno, Rice na Palmer wanamzidi Virgil?”.
Sherehe ya tuz hizo zitafanyika jijini Manchester, Agosti 19.
Van Dijk alikuwa miongoni mwa mastaa wa Liverpool waliocheza vizuri kwa msimu mzima na kukisaidia kikosi hicho cha kocha Arne Slot kunyakua ubingwa. Mashabiki hao walihoji pia kukosekana kwa Ryan Gravenberch, ambaye alikuwa kiungo matata kabisa wa chini kwenye kikosi hicho cha Anfield.
Kuhusu Salah alikuwa bora kabisa, alipofunga mabao 29 na asisti 18, wakati Rice aliisaidia Arsenal kushindania ubingwa, huku Isak alishika namba mbili kwa mabao nyuma ya Salah, akifunga mara 23 kwenye kikosi cha Newcastle. Palmer na Fernandes nao walikuwa kwenye viwango bora kabisa Chelsea na Manchester United mtawalia.