Ureno, Hispania kuti kavu EURO

Monday June 21 2021
spain pic

Munich, Sevilla. TIMU za Ureno na Hispania zimejiweka katika mazingira magumu ya kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano ya Euro baada ya kufanya vibaya katika mechi zao za juzi.

Matokeo ya sare ambayo Hispania iliyapata dhidi ya Poland na kichapo ambacho Ureno walikutana nacho kutoka kwa Ujerumani yameziweka kikaangoni timu hizo na sasa zipo kwenye hatari ya kuaga mapema mashindano hayo.

Timu hizo mbili kila moja inalazimika kuibuka na ushindi katika mechi yake ya mwisho ili ikate tiketi ya kutinga hatua ya 16 bora vinginevyo zitatupwa nje ya mashindano ama kusubiria kupenya kupitia nafasi za ‘best looser’.

Mabingwa mara tatu wa mashindano ya Euro, Hispania walijikuta wakilazimishwa sare ya bao 1-1 na Poland, matokeo yaliyowafanya wafikishe pointi mbili ambazo zimewaweka katika nafasi ya tatu kwenye kundi E na ili wafuzu wanahitajika kuibuka na ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya Slovakia waweze kusonga mbele.

Alvaro Morata alitangulia kuifungia bao, Hispania katika dakika ya 25 lakini dakika ya 54, Robert Lewandowski aliisawazishia Poland huku Gerard Moreno akipoteza fursa muhimu ya kuifanya Hispania kuibuka na ushindi katika mchezo huo baada ya kupoteza mkwaju wa penalti katika dakika ya 58.

Ureno iliyoanza vyema mashindano hayo ilijikuta ikitupwa hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi F baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Ujerumani.

Advertisement

Mabao mawili ya kujifunga ya Ruben Dias pamoja na Raphael Guerrero na mengine yaliyopachikwa na Kai Havertz na Robin Gosens yalitosha kuizima Ureno ambayo mabao yake yalifungwa na Cristiano Ronaldo na Diogo Jota.

Ureno sasa inakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa mwisho wa kundi F na ushindi ndio utawahakikishia kucheza hatua ya 16 bora, lakini sare inaweza kuwapa nafasi ya kupenya kama moja ya timu nne zilizoshika nafasi ya tatu.

Advertisement