Tyson, Joshua ndo hivyo tena

Muktasari:
- Joshua 'AJ' ndiye ataanza kupanda ulingoni mwezi huu dhidi ya Daniel Dubois katika Uwanja wa Wembley, Uingereza huku Fury akikabiliwa na pambano la marudiano Desemba dhidi ya Oleksandr Usyk baada ya Mei, mwaka huu kuchapwa kwa pointi.
LICHA ya mabondia Tyson Fury na Anthony Joshua kuwa na wapinzani wakali zaidi huko mbeleni, ni suala la muda tu kabla ya wao wenyewe kupigana mwakani bila kujali matokeo ya mapambano ya mwaka huu.
Joshua 'AJ' ndiye ataanza kupanda ulingoni mwezi huu dhidi ya Daniel Dubois katika Uwanja wa Wembley, Uingereza huku Fury akikabiliwa na pambano la marudiano Desemba dhidi ya Oleksandr Usyk baada ya Mei, mwaka huu kuchapwa kwa pointi.
Hata hivyo, kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya wasimamizi wao na bosi wa masuala ya burudani nchini Saudi Arabia, Turki Alalshikh, mpango ujao ni kuwapandisha ulingoni Waingereza hao hata kama itatokea wote au mmojawao akapoteza pambano lake mwaka huu.
Kama mpango huo utafanikiwa utakata kiu ya muda mrefu ambayo imekuwapo kwa mabondia hao wenye thamani kubwa zaidi kwa sasa wa uzito wa juu duniani kupanda ulingoni tangu waliporatibiwa kuzichapa 2021, lakini ukafa baada ya Joshua kupigwa na Usyk.