Top 5 kali za kuliamsha NBA

Muktasari:
- Ligi hiyo ambayo imesharudi kwenye kila timu kucheza mechi 82 ili kukamilisha msimu mzima, ina miezi miwili kutokea sasa kabla ya kuanza kusaka wababe wanane wa kila ukanda watakaochuana kusaka taji la NBA ambalo lipo mikononi mwa Boston Celtics iliyolibeba Juni, mwaka huu kwa kuishinda Dallas Mavericks.
TAYARI ratiba ya ligi ndefu (regular season) imeshatolewa mwanzoni mwa wiki hii, ambapo itaanza Oktoba 22 kwa mechi mbili huku moja ikiwa ni ya Ukanda wa Mashariki na nyingine ya Magharibi.
Ligi hiyo ambayo imesharudi kwenye kila timu kucheza mechi 82 ili kukamilisha msimu mzima, ina miezi miwili kutokea sasa kabla ya kuanza kusaka wababe wanane wa kila ukanda watakaochuana kusaka taji la NBA ambalo lipo mikononi mwa Boston Celtics iliyolibeba Juni, mwaka huu kwa kuishinda Dallas Mavericks.
Hapa tunakueletea mechi tano kali za mwanzoni za duru la kwanza ya ligi ndefu ambazo siyo za kukosa kwa wapenzi wa ligi hiyo.
CELTICS VS KNICKS
Huu ndiyo mchezo wa ufunguzi wa ligi ndefu ambao utachezwa Oktoba 22 uwanjani TD Garden ambao ulishuhudia taji la NBA likienda kwa Celtics na kuwa la 18 kwao ikiwa ni rekodi ya jumla katika historia ya NBA.
Boston Celtics dhidi ya New York Knicks unatarajiwa kuwa mchezo mkali sio kwa sababu ya Celtics kupewa pete zao za ubingwa siku hiyo, hapana. Bali ni kutokana na ubora wa timu zote mbili na hususan Knicks ambayo inatarajiwa kuwa na ubora zaidi ya iliyomaliza nao ligi msimu uliopita ikiwa moto.
Ikiongozwa na Jalen Brunson ambaye pia ameongezewa nguvu na staa Mikal Bridges aliyetokea Brooklyn Nets, Knicks inapewa nafasi kubwa ya kushindania ubabe wa Mashariki dhidi ya Celtics inayoongozwa na Jayson Tatum na Jaylen Brown.
NUGGETS VS WOLVES
Mchezo mwingine mtamu na ambao siyo wa kuacha kufuatilia ni baina ya Denver Nuggets itakayokuwa nyumbani kwa Minnesota Timberwolves ya Anthony Edwards na Karl-Anthony Towns ambayo ndiyo iliivua taji Nuggets kabla ya kwenda kupoteza Kwa Dallas Mavericks kwenye fainali ya Magharibi.
Nuggets inayoongozwa na MVP Nikola Jokic na Jamal Murray, na sasa ikiwa na mkali wa triple-double, Russell Westbrook itataka kulipiza kisasi cha kuvuliwa taji na Wolves ambayo kwa sasa ina ubora wa kushindana na timu yoyote NBA.
DALLAS VS WARRIORS
Mchezo huu wa Novemba 12 mbali na kuwa mtamu kutokana na ubora wa timu zote mbili, unaongezwa zaidi utamu na mchezaji Klay Thompson 'Klay Killer' ambaye tangu aanze kucheza NBA mwanzoni mwa 2010 ameitumikia Golden State Warriors kwa kipindi chote kabla ya msimu huu kujiunga na Dallas Mavericks kuungana na wakali Luka Doncic na Kyrie Irving.
LAKERS VS WARRIORS
Hakuna mchezo unaokuwa rahisi kama tu unawahusu mastaa LeBron James dhidi ya Stephen Curry. Mchezo baina ya Los Angeles Lakers na Golden State Warriors utakaochezwa usiku wa Krismas utavuta hisia za wengi kusherehekea sikukuu hiyo kwa patashika ya timu mbili kubwa zenye mastaa wa NBA.
DALLAS VS CELTICS
Huu ni mchezo wa kisasi utakaopigwa, baada ya Mavericks kupewa nafasi kubwa ya kushinda taji la NBA kwa kuwafunga na kuwaondoa wababe Minnesota Timberwolves waliowavua taji Nuggets. Mavericks iliingia fainali ya jumla ya NBA kukipiga dhidi ya bingwa wa Mashariki, Celtics na kuambulia kichapo ikipoteza mechi nne mbele ya Celtics na kuipa taji la rekodi kiulaini bila ushindani uliotarajiwa.
Safari hii bila shaka Mavericks itakuwa na nyongeza ya supastaa Klay Thompson, hivyo itataka kulipiza kisasi mbele ya Celtics ambayo ubora wake umebaki vilevile unaosubiri ligi ianze.
DONDOO
18 - Boston Celtics inaongoza kwa mataji 18 NBA, wao ndio wababe.
25 - Siku ya Krismasi itanogeshwa na mchezo mkali wa Warriors na Lakers.
17 - Lakers ina mataji 17 Moja pungufu dhidi ya Celtics.