Timu tano tishio kwa Celtics msimu ujao

Muktasari:
- Hiyo imedhihirisha ubora wa kikosi ilicho nacho na matokeo yake ikafanikiwa kubeba taji la 18 la NBA lililoipa rekodi kuwa ya kwanza kihistoria kufikisha mataji mengi kuliko timu yoyote. Los Angeles Lakers inaifuatia kwa mataji 17.
KATIKA misimu miwili mfululizo iliyopita timu ya Boston Celtics imecheza fainali ya jumla ya NBA dhidi ya timu za Golden State Warriors na Dallas Mavericks.
Hiyo imedhihirisha ubora wa kikosi ilicho nacho na matokeo yake ikafanikiwa kubeba taji la 18 la NBA lililoipa rekodi kuwa ya kwanza kihistoria kufikisha mataji mengi kuliko timu yoyote. Los Angeles Lakers inaifuatia kwa mataji 17.
Bado mwezi tu kabla ya kuanza kwa ligi ndefu (regular season) inayokwenda kuanza mwezi ujao na hapo ndipo timu zitakapoanza kusaka ushindi wa mechi nyingi zaidi ili kujiweka kwenye nafasi za juu ya msimamo wa Mashariki, itakayozipa faida ya kucheza mechi za nyumbani hatua ya mtoano (playoffs) inayofanya timu kuwa na nafasi kubwa kushinda katika mechi saba za mtoano.
Kulingana na usajili uliofanyika na namna timu zilivyo kwa sasa kuelekea msimu ujao, hizi ndizo timu tano ambazo zinaweza kuivua taji timu hiyo kuanzia Ukanda wa Mashariki kwa kushinda taji la kanda, japo bado Celtics ina nafasi kubwa ya kutetea kama timu mojawapo haitajipanga.
NEW YORK KNICKS
Mechi za kumalizia msimu jana zilikua bora sana kwa timu hii, ilipoongozwa na nyota Jalen Brunson ambaye kazi yake bora ilimwingiza kwenye kuwania tuzo ya MVP wa ligi, kabla pia ya kukabidhiwa unahodha wa timu hiyo, ina nafasi kubwa ya kumaliza utawala wa Celtics msimu ujao kama watarudi na ubora wao wa msimu uliopita. Ongezeko la wachezaji wawili wapya bora, Mikal Bridges na OG Anunoby limeonekana kuiimarisha zaidi timu hiyo na kuwekewa matarajio makubwa ya kuwa wapinzani maradufu wa Celtics ya Jayson Tatum na Jaylen Brown.
PHILADELPHIA 76ERS
Hapo kati timu hiyo ilikuwa na staa James Harden ambaye alitengeneza combo na Joel Embiid, lakini haikudumu baada ya kutolewa kwenye mtoano msimu mmoja nyuma kiasi cha kumfanya Harden ajiondoe kwenye timu isivyotarajiwa na kubaki na Tyrese Maxey ambaye aliboresha kiwango maradufu, lakini kuumia kwa Embiid kuliikosesha ubora timu hiyo.
Habari njema ni usajili wa supastaa Paul George ambaye sasa anaifanya timu hiyo kuwa tishio kwa Celtics kwani ina utatu mkali wa Embiid, Maxey na George ambao kama watakuwa fiti mwanzo mwisho ni tatizo jipya kwa Celtics.
Mbali na George ‘PG13’ Sixers pia imemsajili Guerschon Yabusele aliyeng’ara katika michuano ya olimpiki nchini Ufaransa, akitumikia taifa hilo mwenyeji.
MILWAUKEE BUCKS
Mabingwa hao wa 2021 wa NBA walipofanikiwa kucheza fainali na kuibuka wababe mbele ya Phoenix Suns, bado siyo timu ya kuibeza hata kidogo kutokana na uwepo wa supastaa Giannis Antetokoumpo ambaye kama atakuwa fiti timu nzima inakuwa hatari kwa Celtics na timu pinzani kwenye ligi na hata hatua ya mtoano. Giannis aliye fiti na uwepo wa mkali wa mitupo ya mbali, Damian Lillard ‘Dame’ ni tishio kwa Celtics wakati wowote pamoja na silaha ya pembeni, Khris Middleton, ambaye akiwa fiti ni moto.
MIAMI HEAT
Timu hiyo huwa haina bahati ya kuwekewa matarajio na mashabiki kucheza fainali ya NBA ukiachilia mbali fainali ya Kanda ya Mashariki.
Lakini Heat inayoongozwa na Jimmy Butler haiachi kushangaza na kushtua, kwani ikifika hatua ya mtoano huwa tishio na katika misimu minne iliyopita imecheza fainali mbili kama ilivyo Celtics, lakini fainali zote mbili ilitoka patupu mbele ya Lakers na Denver Nuggets.
PACERS, CAVALIERS
Hizo timu mbili mojawapo inaweza kushangaza mbele ya Celtics kutokana na ubora wa vikosi japokuwa siyo majina tishio kama zilivyo nyingine nne za juu. Indiana Pacers ya Tyrese Haliburton na Pascal Siakam ilicheza fainali ya ukanda dhidi ya Celtics, lakini haikufua dafu na inasubiriwa msimu huu itakuwaje hasa uwepo wa Siakam tangu mwanzo wa msimu.
Upande wa Cleveland Cavaliers inayoongozwa na Donovan Mitchell siyo haba ikiwa na muunganiko mzuri wa wachezaji vijana wenye uchu wa kufanya vizuri kiasi cha kuwekewa matarajio ya kuwa na uwezekano wa kuiweka pembeni Celtics msimu ujao.