Skendo ya kubeti yaibuka AC Milan

MILAN, ITALIA. BEKI wa AC Milan, Alessandro Florenzi anachunguzwa kwa tuhuma za kucheza kamari kinyume cha sheria, wiki kadhaa baada ya Sandro Tonali na Nicolo Fagioli kufungiwa.
Shirika la habari la AGI linaripoti kuwa beki huyo wa kulia wa Milan anatuhumiwa kwa madai ya kucheza kamari huku skendo za kamari zikiendelea Italia.
Nicolo Fagioli anayekipiga Juventus na Sandro Tonali kutoka Newcastle tayari wamefungiwa kucheza soka kwa muda wa miezi na 10.
Florenzi, inaripotiwa, anatarajiwa kukutana na mwendesha mashtaka wa Italia katika siku zijazo kujadili kesi hiyo, lakini anaendelea kuwa kiungo muhimu wa kikosi cha Milan na ameanza kikosi cha kwanza katika mechi tano za Serie A msimu huu, mechi tano akitokea akitokea benchini.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 ana mkataba na Milan wa hadi mwaka 2025 na pia ni mchezaji wa kimataifa wa Italia mwenye uzoefu, akiwa amewakilisha katika mechi 49 na amecheza mechi 49 akiwa na uzi wa Milan tangu alipojiunga mwaka 2022.
Bado haijafahamika kama beki huyo anatajumuishwa kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Fiorentina baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa ambao utachezwa Novemba 25.
Soka la Italia lilikumbwa na kashfa mwezi uliopita baada ya Sandro Tonali, Nicolo Fagioli na Nicolo Zaniolo kutajwa katika uchunguzi na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Italia na Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) kuhusu madai ya kucheza kamari kinyume cha sheria.
Ripoti hizo zinaendelea kudai mashtaka anayokabiliwa Florenzi yanafanana na ya Zaniolo hivyo anachunguzwa kwa kucheza kamari kwenye gemu za kompyuta badala ya soka uwanjani.
Hata hivyo, michezo ya aina hiyo bado inapigwa marufuku kwa wanasoka hususani inapohusisha kamari, lakini adhabu yake huenda ikawa ndogo, huku ripoti ikidai iwapo atapatikana na hatia Florenzi huenda akatozwa faini tu.