Sheikh Jassim hajamalizana na Man United
Muktasari:
- Bilionea Ratcliffe alimpiku tajiri Jassim na nchi yake ya Qatari kwenye mchakato wa kuinunua Man United mapema mwaka huu.
RIYADH, SAUDI ARABIA: BILIONEA Sheikh Jassim bado anaifuatilia kwa karibu Manchester United baada ya tajiri Sir Jim Ratcliffe kupingwa na mashabiki juu ya uamuzi wake anaofanya huko Old Trafford tangu aliponunua sehemu ya hisa za umiliki wa klabu hiyo.
Bilionea Ratcliffe alimpiku tajiri Jassim na nchi yake ya Qatari kwenye mchakato wa kuinunua Man United mapema mwaka huu.
Bilionea huyo wa Kiarabu Jassim aliwasilisha zabuni tano tofauti za kuinunua Man United kutoka kwenye mikono ya wamiliki wake familia ya Glazer, ambao waliamua kuuza sehemu kadhaa ya hisa zao kwa tajiri Mwingereza, Ratcliffe.
Tajiri Ratcliffe na kampuni yake ya Ineos sasa ni wamiliki wa klabu hiyo ya Man United, akisimamia zaidi kwenye masuala ya kisoka, lakini ameripotiwa kuwatibua mashabiki wa timu hiyo kutokana na uamuzi wake wa utata anaofanya kwenye kikosi hicho.
Kwanza alianza kwa kuwafukuza kazi wafanyakazi 250, kisha akapandisha bei ya tiketi za mechi kwa Pauni 66 kabla ya kumfuta kazi aliyekuwa mkurugenzi wa michezo, Dan Ashworth baada ya kumpa kazi hiyo kwa kipindi cha miezi mitano tu.
Mashabiki walianzisha maandamano dhidi ya Ratcliffe katika kuelekea mchezo wa ushindi dhidi ya Everton, huku kikosi hicho kikiendelea kusota kwenye kumi la chini la msimamo wa Ligi Kuu England licha ya kumfuta kazi aliyekuwa kocha wake, Mdachi Erik ten Hag mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa Daily Mail, bilionea Jassim anafuatilia kwa karibu kila kitu kinachoendelea Man United na imeelezwa kuwapo na huzuni na masikitiko makubwa juu ya kufeli kwa mchakato wake wa kuinunua timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.
Bilionea Jassim aliibuka na mpango wake uliofahamika kwa jina la ‘Project Ruby’. Mpango huo ulikuwa na maana kwamba Man United ingetangaza kufutiwa madeni yake yote na ingeondolewa kwenye soko la hisa la New York Stock Exchange siku moja tu baada ya kuchukuliwa na tajiri huyo wa Qatari.
Katika siku ya tatu, Jassim angetangaza mkwanja ambao utatumika kwenye ujenzi wa uwanja mpya. Ratcliffe na kampuni yake ya Ineos wanachelewesha mpango huo wa ujenzi wa uwanja wa Man United hadi majira ya kiangazi ya mwakani, huku kikiundwa kikosi kazi kinachowajumuisha Gary Neville, meya wa jiji la Manchester, Andy Burnham na Lord Coe ambacho bado hakijatoa mapendekezo yake.
Tajiri huyo wa Qatari angeweka mkazo zaidi kwenye kuajiri kuliko kufukuza wafanyakazi na kwamba alikuwa na mpango wa kuwekeza pesa ya kutosha kwenye timu ya wanawake sambamba na kujenga miundombinu mipya ya kufanyia mazoezi na kuwapa mashabiki hisa za klabu.
Sir Alex Ferguson naye angeingizwa kwenye bodi ya washauri endapo kama tajiri Jassim angefanikiwa kushinda zabuni yake ya kuimiliki Man United.
Bilionea Ratcliffe badala yake ameamua kumfuta kazi kocha huyo gwiji Sir Alex Ferguson kwenye nafasi yake ya ubalozi wa klabu. Jassim alipanga pia kujiweka kando kabisa kwenye masuala ya kuingilia masuala ya soka na badala yake angemchukua bosi wa zamani wa Ligi Kuu England, Richard Scudamore kushughulika na masuala ya kuendesha klabu hiyo.
Mpango wa bosi huyo wa Qatari ilikuwa kununua hisa zote Glazers.