Sancho amsubiri Ten Hag aondoke

Muktasari:

  • Kibarua cha Ten Hag kimekuwa kwenye mushkeli mkubwa msimu huu na kumekuwa na imani kubwa huenda akafunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu na miamba hiyo ya Old Trafford itasaka kocha mpya kwa ajili ya kuwaongoza kwenye msimu wa 2024-25.

LONDON, ENGLAND: Staa, Jadon Sancho yupo tayari kurudi Manchester United na kuanza upya maisha yake kwenye kikosi hicho msimu ujao kama tu kocha Erik ten Hag atafutwa kazi mwishoni mwa msimu huu.


Kibarua cha Ten Hag kimekuwa kwenye mushkeli mkubwa msimu huu na kumekuwa na imani kubwa huenda akafunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu na miamba hiyo ya Old Trafford itasaka kocha mpya kwa ajili ya kuwaongoza kwenye msimu wa 2024-25.


Kwa mujibu wa inews, kuondoka kwa kocha Ten Hag kutamfanya Sancho arudi kuendelea na maisha yake ya soka Old Trafford na winga huyo Mwingereza alisema bado hajamaliza kitu anachotaka kufanya kwenye timu hiyo.


Ripoti hiyo inadai Sancho, 24, atakuwa tayari kuanza upya chini ya kocha mpya Man United, lakini hatakuwa tayari kurejea kwenye kikosi hicho endapo kama Ten Hag atabaki kwenye benchi la ufundi.


Sancho alitumika kwenye mechi tatu za kwanza za Ligi Kuu England msimu huu, lakini baada ya hapo alikosekana hasa kwenye ile mechi ya Arsenal, Septemba mwaka jana na kuibuka kwa tatizo kubwa.


Chini ya Ten Hag, itakuwa ngumu sana Sancho kupata nafasi ya kuichezea Man United tena. Lakini, kinachoelezwa ni kuna nafasi finyu sana ya Mdachi huyo kubaki na kibarua chake huko Old Trafford baada ya msimu huu.


Sancho hakuwa na wakati mzuri sana Man United na amefunga mabao 12 na asisti sita katika mechi 82.