Sababu Dalot kujiondoa Ureno

LISBON, ENGLAND. BEKI wa Manchester United, Diogo Dalot na mchumba wake wamebahatika kupata mtoto kwa mara ya kwanza.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 24, alijiondoa katika mechi za kufuzu Euro wiki hii kwa sababu binafsi.

Dalot alimwambia kocha Roberto Martinez kwamba mchumba wake Claudia Pinto alitarajiwa kujifungua kabla ya mechi dhidi ya Liechtenstein.


Kisha aliandika ujumbe wa kumkaribisha mtoto wake wa kike aliyempa jina la Clara kupitia akaunti yake ya Instagram.

Mastaa wenzake wa Man United, Sergio Reguilon na Sofyan Amrabat waliipongeza familia hiyo mpya pamoja na wachezaji wa zamani akiwemo David de Gea na Juan Mata, beki mwenzake wa kimataifa wa Ureno na Man City, Ruben Dias naye alimpa pongezi.

Dalot na Pinto walianza mahusiano tangu mwaka 2020 na alimchumbia Machi, mwaka huu ambapo wanatarajia kufunga ndoa Julai, mwakani.

Beki huyo alitarajiwa kuanza mechi zote mbili za kufuzu Euro 2024 baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na ya Man United, akiwa amecheza mechi 16 katika mashindano yote.

Lakini baada Dalot kujindoa kikosini taarifa ya Ureno ilisema: “Joao Mario ataanza kwa mara ya kwanza akichukua nafasi ya Diogo Dalot kwa sababu ya ishu binafsi baada ya kuwasiliana na Martinez.”