Saa 72 za maombolezo ya Maradona yaanza

Saa 72 za maombolezo ya Maradona yaanza

Muktasari:

  • Jeneza la mkali huyo wa mabao aliyenyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mara moja akiwa na Argentina mwaka 1986 lipo katika makazi ya Rais jijini Buenos Aires, huku ikielezwa leo ungefanyika uchunguzi wa mwili wake kabla ya taratibu za mazishi yake.

WAKATI mastaa mbalimbali duniani wakiomboleza kifo cha gwiji wa soka nchini Argentina, Diego Maradona, serikali ya nchi hiyo imetangaza siku tatu ya maombolezo ya fundi huyo wa mpira aliyefariki dunia jana Jumatano akiwa na umri wa miaka 60.
Rais Alberto Fernández ndiye aliyetangaza siku hizo tatu za maombolezo ambazo ni sawa na saa 72, huku wakazi wa miji mbalimbali nchini humo hususani katika jiji la Buenos Aires, waliopagwa na msiba huo kiasi cha kulazimisha askari kuimarisha ulinzi.
Jeneza la mkali huyo wa mabao aliyenyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mara moja akiwa na Argentina mwaka 1986 lipo katika makazi ya Rais jijini Buenos Aires, huku ikielezwa leo ungefanyika uchunguzi wa mwili wake kabla ya taratibu za mazishi yake.
Maradona, aliyezichezea klabu ikiwemo Barcelona na Napoli, alikuwa nahodha wa Argentina na alishinda Kombe la dunia mwaka 1986 na kufunga bao la kihistoria lililofahamika kama 'Mkono wa Mungu dhidi ya England katika robo fainali, waliyoilaza mabao 2-1.
Kiungo mshambuliaji huyo mapema mwezi huu alifanyiwa upasuaji wa kichwa kuondoa uvimbe kwenye ubongo wake na alikuwa akisubiri kupatiwa matibabu dhidi ya uraibu wa matumizi ya pombe.
Nchini Italia hasa katika mji wa Naples, yaalipo maskani ya klabu ya Napoli aliyoitumia katika mechi 188 na kuifungia mabao 81, mashabiki waliomboleza kwa kuweka maua, kma ilivyo kwenye maskani ya klabu yke ya utotoni ya Argentinos Juniors.

__________________________________________________________________

By Mwandishi Wetu