Pochettino achimba mkwara Chelsea

Muktasari:

  • Kocha huyo wa The Blues alisema inawezekana yeye na benchi lake la ufundi hawana furaha na kusema stresi za matokeo mabaya kwenye timu sio za wamiliki peke yao.

LONDON, ENGLAND: KOCHA, Mauricio Pochettino amesema anaweza kuchagua uamuzi wa kuachana na Chelsea mwishoni mwa msimu huu na kusisitiza kwamba hilo haliwezi kuwa mwisho wa dunia.

Kocha huyo wa The Blues alisema inawezekana yeye na benchi lake la ufundi hawana furaha na kusema stresi za matokeo mabaya kwenye timu sio za wamiliki peke yao.

Pochettino amekuwa kwenye presha muda mrefu tangu alipotua Stamford Bridge kutokana na timu hiyo kuwa na matokeo mabaya ndani ya uwanja.

Kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na PSG mkataba wake umebakiza miezi 12, kulikuwa na wasiwasi huenda akafukuzwa mwisho wa msimu kama Chelsea itaendelea kufanya vibaya. Lakini mambo yamebadilika na mmoja wa wamiliki wa timu hiyo, tajiri Todd Boehly alisema kibarua cha kocha huyo kipo salama wakati wikiendi hii ikiwa na mchezo dhidi ya Nottingham Forest. Hata hivyo, Pochettino, 52, mwenyewe amefichua hatima ya kibarua chake ipo kwenye mashaka, akisema kama kutakuwa na furaha kuanzia kwao hadi kwa wamiliki basi hakutakuwa na shida. “Kama kuna furaha upande wa bosi, basi inapaswa tuulizwe na sisi pia tunakubaliana na hali halisi au tutahitaji kuondoka. Hii haitakuwa mara ya kwanza kwangu na benchi langu la ufundi kuamua kuondoka,” alisema Pochettino.