Pirlo: Sina mpango wa kujiuzulu

Monday May 10 2021
juve pic

TURIN, ITALIA. KOCHA wa Juventus, Andrea Pirlo amesema kwa msisitizo kwamba hana mpango wa kuachana na kibarua  hicho kufuatia kikosi chake kukumbana na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya AC Milani kwenye mchezo wa Ligi Kuu Italia 'Serie A'.

Kipigo ambacho Juventus imekumbana nacho kimewafanya kushuka hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na pointi 69 huku wakizidiwa pointi moja na Napoli ambao wapo nafasi ya nne wakiwa na pointi  70.
 
Licha ya Juventus kugubikwa na wingu jeusi, Pirlo ambaye amewahi kuichezea timu hiyo kwa mafanikio, amesema wala hana mawazo ya kujiuzuru nafasi ya kukinoa kikosi hicho ambacho kilikuwa kikishikilia ubingwa wa Serie A kwa misimu tisa mfululizo.
 
Pirlo amesema, "Kujiuzulu? Hapana siwezi kufanya hivyo. Nilichukua jukumu hili nikiwa natambua kwamba kuna nyakati za raha na shida, bado kuna michezo mitatu mbele yetu, tutapambana ili tumalize nne bora."

Zipo taarifa ambazo bado hazijathibitishwa kwamba huenda muda wowote Pirlo akafutwa kazi kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo ambayo ipo kwenye hatari ya kupoteza nafasi ya msimu ujao kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Advertisement