Pepelu atajwa kumrithi Rodri Man City
Muktasari:
- Pepelu amekuwa akifuatiliwa na maskauti wa Man City kwa muda mrefu na ndio amependekezwa asajiliwe ili kuziba pengo la Rodri.
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amewaambia vigogo wa timu hiyo kwamba anahitaji saini ya kiungo wa Valencia, Mhispania Jose Luis García ‘Pepelu’, 26, kwa ajili ya kuziba pengo la Rodri.
Pepelu amekuwa akifuatiliwa na maskauti wa Man City kwa muda mrefu na ndio amependekezwa asajiliwe ili kuziba pengo la Rodri.
Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote, amefunga mabao mawili na kutoa asisti mbili.
Man City imekuwa katika nyakati ngumu tangu kuanza kwa msimu huu na imepoteza mechi 7 na kushinda mechi moja tu kati ya 10 za mwisho.
Moja kati ya maeneo ambayo inaelezwa yanachangia kushuka kwa kiwango chao ni kiungo cha ukabaji ambapo alikuwa akicheza Rodri anayesumbuliwa na majeraha.
Pepelu ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2028, anaonekana kuwa mbadala sahihi wa Rodri na benchi la Man City.
Alphonso Davies
WAKATI Real Madrid ikidaiwa kujiondoa taratibu katika mchakato wa kutaka kumsajili beki wa pembeni wa Bayern Munich na Canada, Alphonso Davies, 24, imefichuka kuwa Barcelona ipo macho na inataka kumsajili staa huyo mwisho wa msimu.
Davies ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu mbali ya Barca saini yake pia inahitajika na Liverpool.
Thomas Partey
ARSENAL ipo kwenye hatari ya kumpoteza kiungo wake raia wa Ghana, Thomas Partey katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani ambapo atakuwa huru.
Partey ambaye kwa sasa anatumika kama beki wa kulia ni mmoja kati ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa bado hakuna taarifa yoyote juu ya kusaini dili jipya licha ya kuwa mmoja kati ya mastaa muhimu.
Carney Chukwuemeka
TIMU nyingi za Ligi Kuu England zimeendelea kutuma maombi kwenda Chelsea ili kuipata huduma ya mshambuliaji wa timu hiyo, Carney Chukwuemeka, 21, ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Chelsea tangu kuanza kwa msimu huu.
Kati ya timu ambazo zinahitaji saini yake kwa mkopo wa nusu msimu ni Fulham na Crystal Palace.
Richarlison
MSHAMBULIAJI wa Tottenham na Brazil, Richarlison, 27, amepanga kukataa ofa kutoka Fluminense inayotaka kumsajili katika dirisha la majira ya baridi mwakani.
Richarlison ambaye hajaonyesha kiwango bora msimu huu akiwa na Spurs bado anaamini ana nafasi ya kuonyesha makubwa kwenye timu hiyo ya Ligi Kuu ya England.
Rayan Cherki
CRYSTAL Palace inataka wachezaji watatu kutoka Olympique Lyon ambao ni pamoja na mawinga wawili wa kwanza kutoka Ghana, Ernest Nuamah, 21, na kutoka Ufaransa, Rayan Cherki, 21, pia inataka huduma ya beki Sael Kumbedi, 19, ambaye ni raia wa Ufaransa. Mastaa wengi wa Lyon wanadaiwa kutaka kuondoka mwisho wa msimu huu au Januari ili kuepuka kushuka na timu.
Miguel Gutierrez
MANCHESTER United inataka kumsajili beki wa Girona na Hispania, Miguel Gutierrez, katika dirisha la majira baridi mwakani kwa ajili ya kuboresha eneo la ulinzi hususani upande wa kushoto ambako staa huyu anaweza kucheza vizuri.
Gutierrez mwenye umri wa miaka 23, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote.
Victor Lindelof
BEKI wa Manchester United na Sweden, Victor Lindelof, 30, yupo kwenye rada za timu mbalimbali barani Ulaya ikiwemo AC Milan.
Lindelof anatajwa kuwa mmoja kati ya mastaa ambao kocha Ruben Amorim anataka wauzwe katika dirisha lijalo ili kufanikisha uwezekano wa kusajiliwa mastaa wapya katika eneo lao la ulinzi.
Mkataba wa fundi huyu unamalizika Juni mwakani. Msimu huu amecheza mechi mbili tu za michuano yote.