Pep Guardiola atishia kung’atuka Man City

Muktasari:
- Ikiwa inajiandaa kwa mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu mwezi ujao, City imemaliza msimu huu bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2016-17, ambao ulikuwa wa kwanza kwa Guardiola Etihad.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola ameonya ataondoka Manchester City iwapo klabu hiyo haitapunguza idadi ya wachezaji kipindi cha majira ya joto.
Ikiwa inajiandaa kwa mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu mwezi ujao, City imemaliza msimu huu bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2016-17, ambao ulikuwa wa kwanza kwa Guardiola Etihad.
Guardiola amekiri anataka baadhi ya wachezaji waondoke, akisema anapendelea kufanya kazi na kikosi kidogo chenye wachezaji wanaopata nafasi ya kucheza na sio kuwajaza tu jambo linalomfanya kupata wakati mgumu kuwaweka nje baadhi yao.
Baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Bournemouth juzi Jumanne, kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 alisema: “Nimesema kwa klabu sitaki hilo (kuwa na lundo la wachezaji). Sitaki kuwaacha wachezaji watano au sita wamekaa tu. Sitaki hivyo. Nitaondoka. Nipeni kikosi kifupi nitabaki. Ni jambo lisilowezekana kuwaambia wachezaji wakae majukwaani kwamba hawawezi kucheza.”
Savinho, Abdukodir Khusanov, Claudio Echeverri na Vitor Reis, ambao wote walijiunga na City mwanzoni mwa msimu, hawakujumuishwa kwenye kikosi cha mchezo huo wa Premier. Pia vijana waliopitia akademi ya klabu hiyo, Rico Lewis na James McAtee nao walikosa nafasi.
Kwa sasa Man City ina wachezaji 28 wa kikosi cha kwanza, mbali na Kyle Walker, Kalvin Phillips, Joshua Wilson-Esbrand na Maximo Perrone walioko kwa mkopo.
Kuhusu wingi wa wachezaji, Guardiola aliongeza: “Labda kwa miezi mitatu, minne iliyopita hatukuweza kuchagua kikosi cha kwanza, hatukuwa na mabeki, ilikuwa ngumu sana. Baadaye watu walirejea, lakini msimu ujao hauwezi kuwa hivyo.
“Kama kocha siwezi kufundisha wachezaji 24 halafu kila wakati nichague na wengine wanne au sita wabaki nyumbani kwa sababu hawawezi kucheza. Hili halitatokea. Nimesema kwa klabu, sitaki hivyo.”
Kwa sasa City imepata nguvu baada ya wachezaji waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu kama Rodri na Oscar Bobb kurejea uwanjani.
Wakati Guardiola ambaye alisaini mkataba mpya hadi 2027 akilalamikia hilo, kikosi cha Manchester United kina wachezaji 28, Chelsea 31 na Liverpool 24.
Wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza cha Guardiola wana umri wa zaidi ya miaka 30 ambao ni Ederson, Stefan Ortega, Scott Carson, Nathan Ake, John Stones, Kevin De Bruyne, Ilkay Gundogan, Mateo Kovacic na Bernardo Silva.
Jack Grealish na Manuel Akanji nao wanatarajiwa kufikisha miaka 30 katika miezi ijayo.
City imetumia takribani Pauni 200 milioni kwenye usajili msimu huu na inatarajiwa kutumia zaidi msimu huu wa joto.
Ingawa wamehusishwa na kinda wa Lyon, Rayan Cherki, City imeripotiwa kujiondoa kwenye mbio za kumsaini nyota wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz.