Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lewis-Skelly kubeba mikoba ya Partey

Muktasari:

  • Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana, amekuwa mhimili muhimu kwa Kocha Mikel Arteta tangu alipojiunga kutoka Atletico Madrid. Akiwa na umri wa miaka 31, Partey amecheza mechi 51 katika mashindano yote, ingawa Arsenal imemaliza msimu mwingine bila kushinda taji lolote.

LONDON, ENGLAND: IWAPO Thomas Partey ataondoka Arsenal msimu huu wa majira ya joto, huenda kukawa na mabadiliko makubwa katika safu ya kiungo ya klabu hiyo. Mkataba wa Partey unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni, huku hakuna dalili zozote za nyongeza ya mkataba mpya kwa kiungo huyo.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana, amekuwa mhimili muhimu kwa Kocha Mikel Arteta tangu alipojiunga kutoka Atletico Madrid. Akiwa na umri wa miaka 31, Partey amecheza mechi 51 katika mashindano yote, ingawa Arsenal imemaliza msimu mwingine bila kushinda taji lolote.

Mashaka yanaendelea kuongezeka kuhusu uwezekano wa Partey kusalia katika viunga vya Emirates. Hali hiyo imemlazimu kocha Mikel Arteta kuandaa mipango ya dharura ya kumrithi kiungo huyo kikosini.

Uhamisho wa nyota wa Real Sociedad, Martin Zubimendi, bado unazungumzwa, ingawa Real Madrid nayo inaonyesha nia ya kumsajili kiungo huyo wa Hispania, huku kocha anayetarajiwa kutua Bernabeu, Xabi Alonso, akiwa shabiki mkubwa wa mshindi huyo wa Euro 2024 na anatamani kufanya kazi naye katika jiji la Madrid. Hali hiyo inafanya kutokuwa na uhakika kwamba Zubimendi atacheza Ligi Kuu England msimu huu ingawa Arsenal inaamini inaweza kukamilisha dili hilo.

Iwapo Zubimendi hatosajiliwa, basi Arteta anaweza kulazimika kutafuta suluhisho kutoka ndani ya kikosi alicho nacho.

Katika wachezaji wanaotazamiwa ni Myles Lewis-Skelly, ambaye amecheza kikosi cha kwanza msimu huu. Tangu alipoanza kucheza dhidi ya Manchester City, kijana huyo amekuwa chaguo la kwanza la beki wa kushoto kwa Arsenal na hata kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England.

Ingawa amepata nafasi eneo la ulinzi, Lewis-Skelly alikuzwa katika akademi ya Arsenal kama kiungo wa kati na bado anaonekana kuimudu nafasi hiyo. Arteta ni shabiki mkubwa wa kinda huyo kutokana na uwezo wake wa kupokea mpira bila ya presha, anaweza kutumika hapo endapo Partey ataondoka hasa ikizingatiwa kuwa Arsenal tayari ina machaguo kadhaa nafasi ya beki wa kushoto.

Ingawa kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 anaweza kupendezwa na nafasi ya kusogea mbele, hajaonyesha dalili zozote za kutoridhika na nafasi yake ya sasa. Hata hivyo, alikiri yuko tayari kucheza nafasi yoyote ambayo Arteta atampanga.

“Imekuwa safari nzuri kwangu kwa sababu napenda kujifunza na kujiboresha. Nina kiu ya kujifunza kila siku na kukua. Napenda kuuliza maswali. Kama sijui jibu, nitahakikisha nauliza,” alisema Lewis-Skelly na kuongeza.

“Safari imekuwa nzuri kwangu kwa sababu japo mimi ni kiungo kwa asili, nafasi ya ulinzi haikuwa ngeni kwangu. Nimeifurahia. Kwa mtindo wetu wa kucheza, huwa naingia katikati mara kwa mara.

“Nitacheza popote kocha atakapohitaji na ni muhimu kuwa na uwezo wa kucheza nafasi tofauti. Wachezaji bora duniani wanaweza kucheza maeneo mbalimbali. Hivyo, mimi niko tayari kufanya lolote kuwa sehemu ya timu.

“Nataka kuvuka kile ambacho watu wanafikiri ni uwezo wangu. Nataka kuwa bora kila siku. Najiona hilo litanifikisha mbali.”