Hawa wapo kwenye hatari ya kukosa Kombe la Dunia 2026

Muktasari:
- Licha ya Fifa kuongeza timu zitakazoshiriki fainali hizo hadi kufikia 48 kuna wasiwasi na sapraizi kuona baadhi ya nchi zenye majina makubwa na maarufu kwenye fainali hizo kuwa kwenye wakati mgumu kufuzu.
LONDON, ENGLAND: FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zimebakiza mwaka mmoja tu kuanza, lakini utashangaa kuna nchi kadhaa zenye majina makubwa ambazo zimezoeleka kucheza michuano hiyo zinaweza kushindwa kukipiga huko Canada, Mexico na Marekani.
Licha ya Fifa kuongeza timu zitakazoshiriki fainali hizo hadi kufikia 48 kuna wasiwasi na sapraizi kuona baadhi ya nchi zenye majina makubwa na maarufu kwenye fainali hizo kuwa kwenye wakati mgumu kufuzu.
Kutokana na hilo, hizi hapa timu saba maarufu duniani ambazo zitashangaza wengi zikishindwa kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia.
NIGERIA
Unaweza kuwaza ile safu ya ushambuliaji ya timu ya taifa ya Nigeria, yenye wakali matata kabisa kama Victor Osimhen, Ademola Lookman, Victor Boniface, Taiwo Awoniyi na Samuel Chukwueze - lakini bado inataabika kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026. Miamba hiyo ya soka la Afrika, imeshinda mechi moja tu kati ya sita ilizocheza Kombe la Dunia, inaongozwa kwenye kundi na Afrika Kusini kwa tofauti ya pointi sita na haionekani kama itafanikiwa kufuzu kwa tiketi ya timu ya pili bora kwenye kundi.
CAMEROON
Hakuna fainali za Kombe la Dunia zitafanyika bila ya kituko cha Camerooni, kuanzia kwa Benjamin Massing mwaka 1990 hadi kwa Alex Song kupiga mtu kiwiko bila ya sababu yoyote mwaka 2014. Lakini, Cameroon ndiyo nchi ya Afrika iliyoshiriki mara nyingi fainali za Kombe la Dunia, inapata shida kufuzu mwaka huu baada ya kuwa kwenye wakati mgumu mbele ya Cape Verde katika mchakamchaka wa kuwania kufuzu kupitia Kundi D. Ikiwa na mastaa kama Andre Onana, Carlos Baleba na Bryan Mbeumo kwenye kikosi chao, Cameroon iliwachapa wapinzani wao 4-1 katika mechi ya mwanzo mwanzo ya kuwania kufuzu kabla ya kuangusha pointi mbili dhidi ya Libya, Angola na Eswatini. Itakwenda kukipiga na Cape Verde, Septemba mechi ambayo itakuwa kama ya mchujo katika kukamatia tiketi ya fainaoli hizo za Amerika.
SENEGAL
Senegal ilikuwa kivutio kikubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022, ilipovuka kwenye hatua ya makundi na kisha kuonekana kama ingeichapa England kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya kupoteza 3-0. Lakini, mambo yamebadilika kwa haraka kutoka kwenye taifa hilo la Afrika lenye wachezaji wengi wenye vipaji bikubwa. Kocha wa kikosi hicho maarufu kama Simba wa Teranga, Aliou Cisse alifutwa kazi Oktoba 2024 na sasa anainoa Libya, wakati Sadio Mane na Kalidou Koulibaly viwango vyao vinaonekana kushuka huko Saudi Pro League. Senegal ina wachezaji wengi wenye majina makubwa na maarufu kama Pape Sarr na Nicolas Jackson, lakini ipo kwenye hatari kubwa ya kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 ikiburuzwa na DR Congo kwa pointi moja kwenye kundi. Kitakuwa kitu cha kushangaza kuona Senegal haipo kwenye fainali hizo.
QATAR
Sawa, Qatar ilikuwa hovyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizoandaliwa nchini kwao na kuwa nchi ya kwanza mwenyeji kupoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi. Lakini, imefanikiwa kushinda mataji mawili ya mwisho ya Kombe la Asia na kuweka matarajio mengi kuwa safari hii itafanikiwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa nguvu yake na si ya uenyeji. Lakini, mambo yamekuwa tofauti ambapo kikosi hicho cha Qatar kipo kwenye mashaka ya kufuzu. Bado kuna matumaini kiasi kwa Qatar kufuzu kwa sababu ni miongoni mwa timu sita ikiwamo Saudi Arabia ambazo zitacheza kuwania tiketi hiyo ambapo mbili zitatupwa nje.
CHILE
Kama kuna mataifa ambayo mashabiki wangependa kuona yanafanikiwa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia basi ni Chile. Kikosi hicho kimekuwa kikicheza soka la kibishi na kimekuwa na wachezaji mahiri kama ambavyo kilifanikiwa kushinda ubingwa wa Copa America 2015 na 2016 kilipoichapa Argentina ya Lionel Messi kwenye fainali zote mbili. Lakini, huruma ni kwamba kuna wachezaji wengi waliotamba kwenye kikosi hicho cha miaka 10 iliyopita wapo kwenye timu hadi sasa huku kukiwa na vipaji vichache vilivyofikia viwango vya wakali kama Arturo Vidal na Alexis Sanchez. Chile imeshinda mara mbili tu katika mechi 14 za kuwania kufuzuy na sasa inashika mkia kwenye kundi la kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa kupitia Amerika Kusini, ambapo ipo nyuma kwa pointi tano dhidi ya Venezuela waliopo kwenye nafasi ya kucheza mechi ya mchujo. Mbaya zaidi kwa Chile, katika mechi hizo imefunga mabao tisa.
CROATIA
Itakuwa sapraizi kushuhudua taifa lililopata mashabiki wengi wa soka kwa miaka ya karibuni, Croatia kukosa fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kufanya kweli fainali za 2018 na 2022. Shida kubwa kwenye kikosi hicho wachezaji wengi umri umeanza kuwatipa mkono, hivyo huwezi kumtarajia kiungo mwenye umri wa miaka 39, Luka Modric akiwabeba wakali hao kwa mgongo wake. Croatia ipo nyuma kwa pointi sita dhidi ya Czech Republic na majirani zake Montenegro kwenye Kundi L. Kikosi hicho kina wachezaji wa maana kama beki wa Manchester City, Josko Gvardiol, lakini bado kipo kwenye hatari ya kushindwa kufuzu fainali hizo.
AUSTRIA
Baada ya kukosekana kwenye fainali za Kombe la Dunia tangu Ufaransa’98, Austria ilionyesha ubora mkubwa kwenye fainali za Euro 2024 ilipoonyesha kiwango bora chini ya kocha Ralf Rangnick. Ilionyesha ubora mkubwa na kupata ushindi dhidi ya wapinzani wagumu kabisa Poland na Uholanzi kabla ya kwenda kupoteza mbele ya Uturuki katika mechi ya hatua ya 16 bora huku ikicheza soka la kibabe sana. Ikiwa na mastaa wengi wenye vipaji vikubwa na kutamba huko Bundesliga, Austria ilitarajiwa kuwa kwenye nafasi bora ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, lakini mambo ni magumu ambapo imeachwa pointi nyuma ya Bosnia-Herzegovina.