Prime
Kitakachomtokea Pacome Yanga baada ya Aziz KI kuondoka

Muktasari:
- Azizi Ki ameuzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na tayari ameshaondoka nchini kujiunga na klabu hiyo inayojiandaa na Kombe la Dunia la Klabu.
KUONDOKA kwa Stephane Azizi Ki Yanga kumeibua jambo kwa staa wa timu hiyo, Pacome Zouzoua.
Azizi Ki ameuzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na tayari ameshaondoka nchini kujiunga na klabu hiyo inayojiandaa na Kombe la Dunia la Klabu.
Kocha wa Asec Mimosas, Julie Chevalier, ametabiri kitakachomtokea Pacome ndani ya Yanga baada ya kuondoka kwa Azizi KI.
Chevalier amesisitiza kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa Pacome na kama kocha akijipanga vizuri, anakwenda kuwa staa mkubwa klabuni hapo kwa kukiwasha kuliko hata mashabiki walivyokuwa wakimjua.

Amekiri kwamba awali Pacome alikuwa akibanwa kwa kuchezeshwa namba isiyo yake tofauti na alivyokuwa akimtumia Asec.
Mastaa hao wawili waliwahi kucheza pamoja Asec na walikutana tena msimu uliopita katika kikosi cha Yanga, huku Aziz akimtangulia Pacome mwaka mmoja kutua Jangwani.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, kocha huyo wa zamani wa mastaa hao amesema kuondoka kwa Aziz kunaweza kusiwe taarifa nzuri kwa mashabiki wa Yanga, lakini ikawa fursa kwa Pacome.
Amesema uwepo wa mastaa hao katika kikosi kimoja ulikuwa mzuri isipokuwa ulipunguza sana makali ya Pacome, kwani hakucheza kwa kiwango ambacho anakifahamu.
"Ndani ya misimu hii miwili Yanga Pacome bado hajacheza kwa kiwango kikubwa, lakini shida ilikuwa hapati nafasi anayotakiwa kucheza," amesema Chevalier.
"Kama kocha wa Yanga sasa ataanza kumpa Pacome nafasi ya Aziz itakuwa tishio na kiungo huyo atawika kwani hilo ndilo eneo linalomfanya kuwa hatari zaidi."
Ameongeza kuwa," Pacome licha ya kucheza pembeni bado amekuwa hatari kutengeneza na kutumia nafasi, ila natumaini atafanya vyema sana msimu ujao."

Rekodi zinaonyesha kuwa Aziz KI msimu wake wa mwisho 2021/22 ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa kikosi cha Asec na baada ya hapo akatimkia zake Yanga.
Baada ya kuondoka msimu uliofuata 2022/23 Pacome alirithi nafasi hiyo kwa kufunga mabao saba na kuwa mfungaji bora kisha naye akatimkia Yanga.
Na walipokutana Yanga Aziz KI alikuwa akicheza namba 10, huku Pacome akichezeshwa kutokea pembeni kama winga licha ya kwamba Asec alikuwa akitumika kama kiungo asilia yaani namba 10.
Mwanaspoti iliripoti kuwa Aziz KI aliuzwa Wydad kwa Sh2 bilioni na mshahara wake kwa mwezi utakuwa Sh72 milioni.
Yanga pia imeweka vifungu vigumu kwani endapo Aziz KI atakutana na wakati mgumu ndani ya Wydad na kutakiwa kuuzwa au kuondoka, basi mabingwa hao wa Tanzania watapewa nafasi ya kwanza kuzungumza na kiungo huyo.

Kabla ya kuondoka kwa Aziz, Yanga ilishapiga hesabu zake na kuamua kumuongeza mkataba wa miaka miwili Pacome, hivyo msimu ujao huenda akapata nafasi ya kucheza namba 10 kama kocha wake wa zamani anavyoeleza.
MISIMU MITATU YA AZIZ
2022/23-Mabao 09
2023/24-Mabao 21
2024/25-Mabao 09
Misimu hiyo: Asisti 32.
MISIMU MIWILI YA PACOME
2024/25-Mabao 10 na Asisti 09
2023/24-Mabao 07