MZUKA MWINGI: Sterling anavyoleta utamu pale Arsenal

Muktasari:

  • The Gunners imekuwa ikishindania ubingwa kwenye Ligi Kuu England kwa misimu miwili iliyopita, wakijipambanua na kuwa timu ya pili bora zaidi kwenye ligi hiyo.

LONDON, ENGLAND: ARSENAL imekamilisha dili la kunasa huduma ya Raheem Sterling dakika za majeruhi katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, huku usajili huo ukiongeza upana wa kikosi na kupata machaguo ya kutosha kucheza uwanjani.

The Gunners imekuwa ikishindania ubingwa kwenye Ligi Kuu England kwa misimu miwili iliyopita, wakijipambanua na kuwa timu ya pili bora zaidi kwenye ligi hiyo.

Kocha, Mikel Arteta anajaribu kuwa na watu makini kwenye timu yake baada ya kukosolewa kwamba amekuwa hana machaguo ya kutosha kwenye benchi ukiondoa wale wanaoanza kwenye Kikosi cha Kwanza.

Kwa kutazama misimu miwili iliyopita, sehemu kubwa ya mastaa wake kwenye kikosi hicho walicheza kama si mechi zote basi walikaribia kufanya hivyo. Msimu uliopita, Arsenal ilipambana sana, lakini ilikosa huduma za mastaa wachache ambao wangeweza kumalizia kazi kuweza kushindana na Manchester City.

Ujio wa Sterling unakuja kuongeza kitu. Uzoefu wake wa kushinda taji la Ligi Kuu England hilo ni moja, lakini pia mchezaji huyo ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti kwenye fowadi, jambo litakalomruhusu kocha Arteta kukibadili kikosi chake kulingana na mpinzani kwa kuwa atakuwa na machaguo ya kutosha yasiyopungua mawili kwenye upangaji wa timu yake na mfumo. Staa huyo aliyetua kwa mkopo Emirates akitokea Chelsea yupo tayari kuongeza kasi kwenye kikosi hicho ligi itakaporejea baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa. Hakucheza mechi za kwanza kwenye ligi, hivyo Arsenal inataka kuhakikisha anakuwa fiti kwanza kabla ya kupewa gwanda na mtutu kuingia kwenye uwanja wa vita.

Mmoja wa wachezaji watakuwa na faida kubwa kwa ujio wa Sterling ni Bukayo Saka - kwa sababu atapata muda wa kupumzika na kuchaji betri yake tofauti na ilivyo kwa sasa anavyocheza karibu kila mechi kwa msimu mzima.

Arsenal haikuwa na mtu wa maana kwenye upande wa wingi ya kulia, hivyo jambo hilo lilimfanya Saka atumike muda wote.

Hivyo, Sterling atakuja kumpunguzia Saka presha ya kuwa uwanjani kwenye kila mechi.

Kingine ni kwamba Sterling anawapa Arsenal faida ya winga anayetumia mguu wa kulia kucheza upande huo tofauti na Saka, anayetumia mguu wa kushoto, ambapo wakati mwingine anashindwa kupiga krosi ya moja kwa moja kwa mshambuliaji wa kati.

Ilikuwa rahisi kumkariri Saka anapokuwa na mpira upande huo, kwa sababu ni lazima atahitaji kuingia ndani ili kupata unafuu wa kutumia mguu wake wa kushoto.

Kocha Arteta, kwa nyakati nyingi anaweza kumtumia Sterling kama mshambuliaji wa kati.

Na kutokana na ukweli kwamba Arsenal haijasajili Namba 9 kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, eneo ambalo hakika lilihitaji kuboreshwa, Sterling sasa na Kai Havertz wanaweza kusaidiana na Gabriel Jesus kwenye namba yake halisi kwenye eneo hilo.

Havertz anaweza kutumika kwenye Namba 10 kama Sterling atatumika kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati, huku jambo hilo likimfanya Martin Odegaard kupata muda wa kupumzika kutafuta nguvu mpya tofauti na sasa anavyocheza karibu kila mechi.

Chaguo jingine la Sterling, kocha Arteta anaweza kumtumia kwenye Namba 10 na kisha Havertz akacheza kwenye Namba 9, huku Odegaard akipata muda wa kupumzika.

Havertz, ambaye alifunga kwenye mechi ya sare ya Brighton, amekuwa akichezea nafasi ya mshambuliaji wa kati, lakini pia Sterling anaweza kucheza hapo kwa kuwa kuna nyakati kocha Pep Guardiola alikuwa akimtumia kama Namba 9 bandia, huku Manchester City.

Kingine, ambacho Sterling anaweza kukipeleka kwenye kikosi hicho cha Emirates ni kucheza upande wa kushoto, atakapobadiliana na Gabriel Martinelli na Leandro Trossard. Hilo linamfanya Arteta kuwa na machaguo ya kutosha kwenye upande huo wa uwanja, kwamba atakuwa anatua chuma na kuingiza chuma.